MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- KUFUNGUA TAMASHA LA UTAMADUNI-MAHONDA - KWA NIABA YA RAIS WA ZANZIBAR


 

 

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo itaendelea kuweka Mazingira bora ya kuendeleza sanaa na utamaduni wa Mzanzibari nchini kwa maslahi mapana  ya vizazi vya sasa na baadae.  

 Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Mwinyi katika hafla ya ufunguzi wa Tamasha la ishirini na Tisa ( 29 ) la Utamaduni wa Mzanzibari lililofanyika katika  uwanja wa Misuka Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 Amesema Serikali tayari imeanza ujenzi wa nyumba ya Sanaa Mwanakwerekwe kwa lengo la kuviendeleza vipaji vya wasanii na wajasiriamali wanatengeneza bidhaa za utamaduni ambapo litakapomalizika litatumika kwa kufundishia sanaa mbali mbali na vitu vya utamaduni ambavyo vitasaidia kuitangaza Zanzibar nje ya nchi sambamba na kutoa fursa kwa wahitimu kuweza kujiajiri wenyewe.

 Mhe. Hemed amesema Sekta ya Utalii inaendelea kukuwa kwa kasi kubwa visiwani Zanzibar na kutoa nafasi kwa Wazanzibari kuzitumia bidhaa za kiutamaduni na vyakula vya asili ambavyo vinawavutia watalii wengi wanaongia na kutoka Zanzibar na  kuchangia kuongezeka kipato kwa mtu mmoja mmoja Nchi kwa ujumla.

 Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameielekeza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwaandaa mapema walimu wenye sifa na uwezo ambao watakaoutumia kuwafundisha vijana na kuweza  kutambulika duniani kote paamoja na kuweza kuajiriwa katika Mahoteli, Makampuni binafsi na Serikalini.

 Sambamaba na hayo Mhe. Hemed amewahakikishia wazanzibari kuwa Serikali itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano ambao utahitajika katika kufanikisha maadhimisho ya Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari na matamasha mengine ili kuenzi na kudumisha fikra na falsafa za waasisi wa taifa hili.

 Nae waziri wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe.Tabia Maulid Mwita amesema Wizara ya Habari kupitia Idara ya Utamaduni na Sanaa imekuwa ikitoa elimu juu ya kulinda Utamaduni wa Mzanzibari kupitia TV, Radio na mitandao ya kijamii kwa lengo la kuhakikisha Mila, Silka na utamaduni wa Mzanzibari unaendelea kulindwa na kudumishwa vizazi na vizazi.

 Aidha Mhe. Tabia amesema Wizara ya Habari haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kutokulinda na kuvunja Utamaduni za Mzanzibari ambao umekuwa ukiitangaza Zanzibar kupitia sanaa mbali mbali .

 Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini "B" Ndugu Hamid Seif Said amesema Mkoa wa Kaskazini Unguja umetekeleza utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Mapinduzi kwa zaidi ya asilimia mia kwa kujengwa miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo Afya, Elimu, miundombinu ya barabara na masoko ya kisasa.

 Mhe. Hamid amesema Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari linatoa somo na fundisho kwa vizazi vya sasa juu ya kutunza na kudumisha Utamaduni, Mila na Silka za Mzanzibari kwa faida ya Taifa.

 Mapema Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar alipokea maandamano ya wasaniii mbali mbali sambamba na kukagua mabanda ya mauonesho ya wasanii na wajasiriamali waliofika katika ufunguzi wa tamasha hilo.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kutajenga hospitali ya Mkoa maeneo






SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itajenga hospitali kubwa ya Mkoa maeneo ya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa Kaskazini Unguja ambayo itafadhiliwa na Serikali ya Oman.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Utawala na Fedha, Khalid Almuslahi.

Dk. Mwinyi amesema ujenzi wa hospitali hiyo ni muhimu kwa dhamira ya Serikali ya kuwa na hospitali kubwa kwa kila Mkoa ili kuwafikishia wananchi huduma bora karibu na makaazi yao na kupunguza msongamano kwenye hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.

Rais Dk. Mwinyi ameipongeza Serikali ya Oman kwa kushiriki kikamilifu kwenye miradi ya Maendeleo hapa nchini kwa taasisi mbalimbali za nchi hiyo kuiunga mkono Zanzibar kiufundi na kitaalamu.

Dk. Mwinyi alimuhakikishia Naibu Waziri huyo kwamba uhusiano uliopo baina Zanzibar na Oman upo imara, hivyo Miradi ya ushirikiano inayoendelea itaweka alama zaidi katika kudumisha uhusiano wa diplomasia baina ya pande mbili hizo.

Akiuzungumzia Mji Mkongwe wa Zanzibar, alisema kuwa ni eneo muhimu la urithi, linalohitaji kuendelezwa wakati wote, hivyo juhudi zinazofanywa na Serikali ya Oman ya kuukarabati na kuuimarisha ni kuunga mkono juhudi za Serikali kuinua Uchumi wa nchi.

Alisema, Mji Mkongwe mbali ya kuwa kivutio cha utalii pia ni eneo muhimu la kukuza Uchumi na utamaduni wa Zanzibar na Serikali itaendelea kuchukua juhudi mbalimbali za kuutunza mji huo. 

Serikali ya Oman katika kuendeleza ushirikiano wake na Zanzibar inafadhili miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali, ukarabati wa Mji Mkongwe, huduma za maji na umeme na Elimu.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.


POLISI ZANZIBAR YAMDAKA TAPELI KWA KUJIZOLEA MILIONI 6 AKIJIFANYA ANANAFASI YA KAZI YA USALAMA WA TAIFA


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi ACP Abubakar Khamis Ally akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisini kwake Madema, Zanzibara. 

..........................

Polisi, Zanzibar

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linamshikilia Marco Daud Zagamba (32) wa Mbweni, kwa tuhuma za kujipatia sh. milioni 6 kwa njia ya utapele wa kuwapatia ajira watu mbalimbali kati Idara ya Usalama wa Taifa na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Madema, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi ACP Abubakar Khamis Ally amesema mtuhumiwa huyo aliwatapeli wananchi kwa kuwaahidi kuwapatia ajira kwenye Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Idara ya Usalama wa Taifa.

Amefafanua kwamba mtuhumiwa huyo hutumia mbinu ya kujifanya mtumishi wa Serikali na kuwa ana uwezo wa kutoa ajira ambapo alifanya hivyo akijua kuwa ni kinyume cha sheria.

Ametoa mwito kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya watuhumiwa wa utapeli hasa kipindi hiki ambacho Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP. Camillus Wambura ametangaza usaili kwa waombaji wa ajira za Jeshi la Polisi.

Makamu wa Rais ahimiza maadili ili kuvutia jamii kushiriki michezo, mazoezi.













ZANZIBAR.

MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Othman Massoud Othman amevitaka vikundi vya mazoezi nchini kuweka kanuni na miongozo ya maadili ambayo itasaidia kuondoa mitizamo hasi kwa jamii juu ya ushiriki wa makundi yote katika vikundi vya mazoezi na michezo.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na vikundi vya mazoezi katika halfa ya kuhamasisha ushiriki wa jinsia zote kwenye mazoezi na michezo ikiwa ni  maadhimisho ya kutimia miaka kumi ya klabu ya mazoezi Gombani kisiwani Pemba.

Alisema, kuwepo kwa kanuni zinazosimamia maadili katika mazoezi na michezo kutasaidia watu wengi hasa wanawake kuona eneo hilo ni salama kwao na kuondoa dhana potofu iliyojengeka katika jamii.

Alieleza, "niwaombe tuweke kanuni za kusiamamia maadili zitakazo ondoa dhana potofu kwa jamii ili tuweze kuwavutia watu wengi kushiriki mazoezi kwasababu hili jambo ni jema zaidi."

Aidha, makamu huyo wa kwanza wa Rais ambaye aliongoza matembezi na mazoezi ya wanamichezo hao alifahamisha kuwa taifa linapata hasara kubwa kugharamia matibabu ya maradhi yasiyoambukiza yanayosababishwa na mfumo wa maisha ambapo iwapo jamii itakuwa na mwamko wa kushiriki katika mazoezi na michezo itasaidia kupunguza gharama hizo.

"Jambo hili ambalo mnaliendeleza kwetu sisi wengine linatupa faraja sana kwasababu tunajua mnafanya jambo kubwa kwa jamii na nchi yetu kwani kama kuna jambo ambalo nchi inapata hasara ni kwenye matibabu. Na matibabu ya maradhi yasiyoambukiza kwahakika ni ya ghali sana na nyinyi nyote ni mashahidi," alieleza, Mhe. Othman Masoud.

Katika hatua nyingine alihimiza jamii kupewa elimu ya matumizi lishe ili kujiepusha na ulaji holela unaopelekea athari kiafya.

Mhe. Othman Masoud alisema, “twende mbali zaidi kutoa ya elimu ya lishe kwa jamii. Kwasababu hili wengi bado huko tuna tatizo. Tumeacha sasahivi vyakula asilia. Mwingine anaona pengine vyakula asilia sio usasa. Lazima twende katika hatua ya kujitunza na kujipenda kwa kutambua kipi kibaya na kipi kizuri cha kula.”

Naye Mkuu wa wilaya ya Chake chake, Abdalla Rashid amemshukuru Mhe. Othman kwa kuwa miongoni mwa washiriki katika bonanza hilo na kuwahimiza wananchi kuhakikisha kwamba wanahamasishana ili wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi katika kujiepusha na maradhi mbalimbali yasiyoambukiza.

Akitoa salamu za wadau, afisa programu ya michezo kwa maendeleo kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Khairat Haji alieleza bado kuna changamoto kwenye jamii ya uelewa kuhusu umuhimu wa mazoezi na kupelekea vikwazo kwa makundi yote hasa wanawake kushiriki kikamilifu katika mazoezi na michezo.

Aidha aliongeza, ukosefu wa miundombinu na vifaa wezeshi vya mazoezi ni kikwazo katika ufikiaji wa usawa wa kijinsia kkwenye michezo na kuomba serikali na wadau kusaidia kuboresha miundombinu hiyo ili kuwezesha kila mmoja kushiriki bila kikwazo.

"Kuna changamoto kadhaa ambazo tumeziona ikiwemo ukosefu wa vifaa na miundombinu wezeshi kwaajili ya makundi yote kushiriki katika michezo mbalimbali," alifahamisha afisa huyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa klabu ya mazoezi Gombani, Hamad Malengo aliomba wadau kuungana pamoja kushiriki katika michezo na mazoezi ili kuondoa dhana hiyo potofu iliyojengeka katika jamii kuwa kushiriki michezo ni kujifunza uhuni.

Alisema, "elimu kwa jamii inahitajika zaidi ili kutoa mwamko wa watu kushiriki kwenye mazoezi na kuachana na dhana kwamba michezo ni uhuni. Ni lazima tusimame pamoja ili kila mmoja wetu aweze kushiriki mazoezi kwaajili ya afya yake.”

Hafla hiyo ya kuhamasisha ushiriki wa jinsia zote kwenye mazoezi na michezo ikiwa ni maadhimisho ya kutimia miaka kumi ya klabu ya mazoezi Gombani kisiwani Pemba iliyoandaliwa kwa kushirikiana na TAMWA-ZNZ na Shirika ka Bima la Zanzibar  imevishirikisha vilabu zaidi ya vitano vya mazoezi kutoka Unguja, Tanga na wenyeji Pemba.

RAIS WA ZANZIBAR ALHAJJ DK.HUSSEIN ALI MWINYI AMEJUMUKA NA WANAFAMILIA NA WANANCHI KATIKA MAZIKO YA MAREHEME ZULEKHA AHMED ABDALLAH

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussei Ali Mwinyi  akijumuika na Viongozi wa Serikali, Dini na Wananchi katika maziko ya aliyekuwa Mke wa Marehemu Sheikh.Hyder Jabir Saleh E-Farsy,Marehemu Zulekha Ahmed Abdallah,yaliyofanyika katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar .(Picha na Ikulu).
 

RAIS WA ZANZIBAR MHE.DK.HUSSEIN MWINYI AZUNGUMZA NA UJUMBE KUTOKA JIMBO LA SHANDONG CHINA IKULU ZANZIBAR.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Mhe.Zhang Xinwen Makamu Mwenyekiti wa (CPPCC) kutoka Jimbo la Shandong Jamhuri ya Watu wa China, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 17-7-2024.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe kutoka Jimbo la Shandong Jamhuri ya Watu wa China, ukiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa (CPPCC) Mhe.Zhang Xinwen (kulia kwa Rais) akiwa na ujumbe wake,mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 17-7-2024.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi ya mlango wa Zanzibar mgeni wake Makamu Mwenyekiti wa (CPPCC) kutoka Jimbo la Shandong Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Zhang Xinwen, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 17-7-2024.(Picha na Ikulu)

RAIS WA ZANZIBAR MHE.DK.HUSSEIN ALI MWINYI AMEFUNGUA TAMASHA LA MWAKA KOGWA MAKUNDUCHI MKOA WA KUSINI UNGUJA LEO 16-7-2024


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akipata maelezo ya vyakula vya asili kutoka kwa Mzee wa Makunduchi Bi.Amina Ubwa Ali,baada ya kulifungua Tamasha la Mwaka Kogwa 2024, linalofanyika katika viwanja vya Kae Kuu Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja  16-7-2024.na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud.(Picha na Ikulu)

RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHE.DK.HUSSEIN MWINYI AMEIFUNGUA BUSTANI YA MNAZI MMOJA MJI MKONGWE JIJINI ZANZIBAR LEO


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kuifungua Bustani ya Mnazi Mmoja Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar, iliyoko jirani na Hospitali ya Mnazi Mmoja, ufunguzi huo uliyofanyika leo 15-7-2024, na (kulia kwa Rais) Mwenyekiti wa Kampuni ya Infinity Group Bw. Samuel Saba na ( kushoto kwa Rais) Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga.(Picha na Ikulu)

RAIS WA ZANZIBAR MHE.DK.HUSSEIN MWINYI AMEUFUNGUA MKUTANO WA WAZALISHAJI WA SUKARI WA NCHI ZA SADC UKUMBI WA HOTELI YA GOLDEN TULIP UWANJA WA NDEGE ZANZIBAR


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuufungua Mkutano wa Wazalishaji wa Sukari katika Nchi SADC, ufunguzi huo uliyofanyika leo 10-7-2024 katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa TUZO Maalum na Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Sukari Tanzania (TSPA)Bw.Seif Ali Seif, baada ya kuufungua Mkutano wa Wazalishaji wa Sukari kwa Nchi za SADC, unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar leo 10-7-20214.(Picha na Ikulu)

DKT. JAFO AAHIDI USHIRIKIANO KWA WAFANYABIASHARA


WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo (Mb) ameihakikishia sekta binafsi hususani Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Viwanda kuwa watapata ushirikiano mkubwa katika kutatua changamoto mbalimbali za kibiashara ili kuhakikisha wanafanya biashara kwa chini ya uongozi wake.

Ameyasema hayo Julai 5, 2024, alipokuwa akizungumza na baadhi ya Taasisi zilizochini ya Wizara yake zinazofanya kazi kwa ushirikano kati ya Tanzania Bara na visiwani zinazohusika na masuala ya biashara mara baada ya hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu ndogo Tunguu, Zanzibar,

Aidha Dkt Jafo ametiwa wito kwa Wizara za Kisekta na sekta binafsi Bara na Visiwani kushirikiana kwa karibu na Wizara yake ili kukuza Sekta ya Viwanda na Biashara na kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan inayo.

Vilevile, ameahidi kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali wakabili wafanyabiasha, wamiliki wa viwanda na sekta binafsi kwa ujumla inayoajiri watu wengi zaidi nchini ili kuongeza ajira, pato la taifa na kujenga uchumi imara na shindani wa viwanda.

Dkt. Jaffo pia amesema akiwa pamoja na wataalamu wake ataendelea kukutana na wafanyabiashara mbalimbali kupitia mabaraza ya biashara katika mikoa yote nchini kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kujipanga jinsi ya kuzitatua ili kuhakikisha sekta ya viwanda na biashara inakua na kuongeza ajira, Pato la Taifa na kujenga uchumi imara na shindani.

Aidha, ameagiza kila Mtumishi wa wa Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Taasisi zake kutimiza wajibu wake kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha Wizara hiyo inafikia matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza Sekta ya Viwanda na Biashara.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil T. Abdallah akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Bi Fatma Mabrouk Khamis wamemuahidi Waziri Jaffo kuwa wako tayari kushirikiana naye katika kutekekeza majukumu na maelekezo yote yaliyotolewa kwa wizara hizo ili kufikia malengo tarajiwa










TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA IKULU, ZANZIBAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Kampuni ya ‘Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” kutoka nchini China kwa uamuzi wake wa kuja kuekeza hapa Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” kutoka nchini China ambayo imedhamiria kuekeza katika kiwanda cha Makonyo, kilichopo Wawi Pemba kwa kushirikiana na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliihakikishia Kampuni hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushirikiano wake mkubwa kupitia Wizara yake ya Biashara na Viwanda pamoja na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” chini ya Mwenyekiti wake Zhou Junxue kwa kusaini Makubaliano ya Awali kati ya Kampuni hiyo na Shirika la (ZSTC).

Aidha, Dk. Shein aliueleza ujumbe wa Kampuni hiyo kuwa Kiwanda cha Makonyo kilichopo Wawi ni cha muda mrefu ambacho kimekuwa kikizalisha mafuta ya aina mbali mbali hivyo, ushirikiano wa pamoja katika uzalishaji kiwandani hapo kutasaidia kuinua ubora wa kiwanda sambamba na kuongeza pato la Taifa na soko la ajira.

Alieleza kuwa uwamuzi wa Kampuni hiyo ni mzuri na umekuja katika wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, hivyo hatua hiyo itakuwa chachu katika kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na viungo vya vyakula vya aina nyingi ambavyo miongoni mwao vimekuwa vikitoa mafuta bora ambayo yamekuwa ni bidhaa muhimu iliyoingia katika soko la ndani na nje ya Tanzania yakiwemo mafuta ya makonyo, mafuta ya karafuu na  mafuta ya mikaratusi.

Hivyo, Dk. Shein aliongeza kuwa kuanza kwa uwekezaji huo kutazidi kuitangaza Zanzibar na kuwa kiwanda cha pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kinachozalisha bidhaa hizo za mafuta.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya Kampuni hiyo kushirikiana na ZSTC katika kutekeleza makubaliano hayo yaliotiwa saini hapo jana ikiwa ni pamoja na kuongeza zaidi uzalishaji huku akisisitiza suala zima la ufanyaji utafiti katika kilimo cha mazao hayo yanazotoa mafuta.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza suala la mafunzo ambalo litasaidia sana kuendesha kiwanda hicho pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za aina mbali mbali za mafuta ya viungo kutoka katika kiwanda hicho cha Makonyo Wawi jambo ambalo pia, litaongeza soko la ajira hapa nchini.

Nae Mwenyekiti wa Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya China, Zhou Junxue alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar kwa kupitia sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vidogo na vya kati.

Mwenyekiti wa Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” alimueleza Rais Dk. Shein mikakati iliyowekwa na Kampuni yake katika kuhakikisha makubaliano waliyosaini yanatekelezwa kwa lengo la kuleta manufaa kwa pande zote mbili.

Junxue alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Kampuni yake itatoa mashirikiano makubwa kwa Serikali kupitia Shirika lake la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuhakikisha kiwanda hicho kinatoa mafuta yalio bora sambamba na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazozalishwa katika kiwanda hicho cha Wawi.

Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya nchini China ambayo ndio mnunuzi mkubwa wa mafuta ya viungo vya Zanzibar tokea Julai mwaka 2017, ilitiliana saini Makubaliano ya Awali na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuendesha mradi ndani ya miaka kumi utaohusisha uimarishaji wa utendaji na utaalamu katika kiwanda cha Makonyo Wawi.

Jambo jengine ni uendelezaji wa mazao ya karafuu na mikaratusi ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 60 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia tani 2,000,
ubadilishanaji uzoefu kati ya watendaji wa taasisi hizo, upatikanaji wa mafunzo, mbinu na upatikanaji  mbegu bora za mikaratusi ni miongoni mwa makubaliano hayo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
 
 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa