Home » » CUF yataka wahamiaji haramu Zanzibar

CUF yataka wahamiaji haramu Zanzibar

Chama cha  Wananchi (CUF) kimeishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuendesha zoezi la kuwasaka wahamiaji haramu  visiwani  Zanzibar kutokana na kuwapo kwa  wimbi la wahamiaji hao ili kuweza kupunguza vitendo vya uhalifu ikiwemo matumizi ya mabaya ya tindikali.

Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi wa Mawasiliano, Habari na Haki za Binadamu wa chama hicho, Salum Bimani, jana.

Alisema  Tanzania ni nchi mbili zilizoungana hivyo zoezi la kuwasaka wahamiaji haramu linapaswa kuendeshwa nchi nzima na si kwa Tanzania Bara pekee kwani wahamiaji haramu wameenea katika pande zote hususan katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema chama hicho kimeunga mkono  zoezi  la kuwasaka wahamiaji haramu linaloendelea Tanzania Bara hivyo zoezi hilo kuihusisha na Zanzibar kwani litasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu ikiwemo  matumizi mabaya ya tindi kali ambayo yameshamiri visiwani Zanzibar.

“Inashangaza kuona zoezi la kuwasaka wahamiaji haramu linafanywa Tanzania Bara peke wakati sisi ni nchi mbili zilizoungana  kuunda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Bimani.

Chama hicho kimetoa agizo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kulifanyia kazi suala hilo ili  zoezi hilo lisaidie haki kutendeka kwani tayari kuna fununu kwamba baadhi ya wahamiaji haramu waliopo Zanzibar wameshapatiwa vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi na upo uwezekano wa kupiga kura mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hamad Masoud, aliitaka Zanzibar pamoja na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kulifanyia uhakiki daftari la Wapigakura kabla ya uchaguzi mkuu kutokana na alichodai kuwa daftari hilo lina  kasoro nyingi ikiwamo watu wasiokuwa na sifa ya kuandikishwa wameandikishwa katika  daftari hilo .
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa