Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anaondoka Nchini leo jioni kuelekea
Washington kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye
asili ya Afrika ya Kaskazini Magharibi mwa Picific unaotarajiwa
kufanyika katika Jimbo la Seattle Nchini Marekani.
Balozi Seif amepata
heshima hiyo kufuatia ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye asili
ya Afrika kutoka Marekani uliowahi kufanya ziara hapa Zanzibar kati
kati ya mwezi wa April Mwaka huu na kujionea mazingira mazuri ya
uwekezaji jambo ambalo Zanzibar imepatiwa fursa ya kwenda kujitangaza
Nchini humo.
Mtandao wa Jumuiya ya
Wafanyabiashara wenye asili ya Afrika Nchini Marekani umeamua kufungua
ukurasa mpya katika kuona inaendeleza mashirikiano na Nchi rafiki
ikilenga kusaidia taaluma na hata uwezeshaji kwa Taasisi na Mashirika
Barani Afrika ili yajinyanyue kiuchumi.
Katika ziara hiyo ya
wiki moja ya Kiserikali itakayotoa pia fursa ya kutembelea baadhi ya
Makampuni na Taasisi za Umma, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
anauongoza ujumbe wa Viongozi saba wa Serikaliwakiwamo Mawaziri,
Watendaji wa serikali na Maafisa waandamizi.
Viongozi anaofuatana
nao ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed, Waziri wa Biashara
Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazrui pamoja na Mwakilishi wa Jimbo
la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma.
Wengine ni Mwenyekiti
wa Chama cha wafanyabiashara Zanzibar Abdulla Abass, Katibu Mkuu Wizara
ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ali Khalil Mirza, Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu Abdulla Mzee Abdulla,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Bahari Kuu Zahor Mohammed El- Kharousy pamoja na timu ya wafanyabiashara
wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake akiambatana na baadhi ya
wafanyabaiashara maarufu hapa Zanzibar atapata fursa ya kutembelea
Kampuni ya utengenezaji wa ndege za Abiria na mizigo ya Boeing Mjini
Seattle, kukutana na Uongozi wa Mfuko wa misaada wa Melinda Gates na ule
wa Microsoft pamoja na jumuiya ndogo ndogo za wafanyabiashara.
Maeneo mengine
watakayopata fursa ya kutembelea ni ni baadhi ya Taasisi za Serikali,
Meya wa Jiji la Seattle ziara iakayoambatana pia na vikao na Mikutano ya
Wafanyabiashara wa Zanzibar na Mji huo katika kubadilishana mawazo na
kuanza kupanga mikakati ya ushirikiano.
Aidha Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar amepanga kukutana na Wanachama wa Jumuiya ya
Wazanzibari na Watanzania wanaoishi Mjini Seattle na Washington kwenye
Tafrija maalum waliyojipanga kumuandalia yeye na ujumbe wake
aliofuatana nao.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif anatarajiwa kukamilisha ziara yake Mjini
Seattle Nchini Marekani Mnamo Tarehe 14 Novemba 2013 na kurejea nyumbani
kwa kupitia Dubai.
Mapema asubuhi kabla
ya kuondoka Nchini kuelekea Marekani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Balozi Mdogo mpya wa Jamuhuri ya Watu
wa China hapa Zanzibar Bwana Xie Yunliang ambae alifika kujitambuluisha
rasmi.
Katika mazungumzo yao
yaliyofanyika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini
Zanzibar Viongozi hao walielezea haja ya pande hizo mbili kuendelea
kushirikiana katika miradi ya maendeleo China ikiwa mshirika mkubwa wa
Zanzibar katika uimarishaji uchumi na ustawi wa Jamii.
Balozi Xie Yungliang
alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba China itaendelea
kuunga mkono harakati z maendeleo za Zanzibar katika kujiletea maendeleo
na kupunguza umaskini.
Alisema China ilitenga
zaidi ya Yuan Milioni Mia moja katika kuunga mkono miradi ya Skuli,
awamu ya Pili ya ujenzi wa uwanja wa ndege bwa Kimataifa wa Zanzibar
Kisauni pamoja na ile awamu ya Pili ya mradi wa Mkongo wa Mawasiliano
hapa Zanzibar.
Naye akitoa shukrani
zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza
Jamuhuri ya Watu wa China kwa jitihada zake za makusudi za kuona
Zanzibar inajikwamua kutoka katika wimbi la umaskini.
Balozi Seif alimuahidi
Balozi huyo Mdogo mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kumpa ushirikiano wa karibu katika
utekelezaji wa majuku yake aliyopamngiwa na Nchi yake.
Baadaye Balozi Seif
pia alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar Bwana
Saleh Suleiman Al - Harith ambae naye alifika kujitambulisha bada ya
kuteuliwa na Nchi yake kufanya kazi ya Kidiplomasia hapa Zanzibar.
Mazungumzo yao
yalijikita zaidi katika kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati
ya Nchi hizo ambao ni wa kihistoria kutokana na maingiliano ya kidamu ya
wananchi wa pande hizo mbili.
Balozi Seif alimueleza
Balozi Mdogo wa Oman Nchini kwamba Zanzibar Zanzibar inahitaji kuwa na
viwanda vidogo vidogo hasa vya matunda ilikuweza kusaidia uchumi wake.
Alisema wananchi wengi
hasa wakulima wamekuwa wakizalisha idadi kubwa ya matunda ambayo
baadaye hupotea na kuleta hasara kutokana na wakulima hao kukosa
utaalamu wa hifadhi ya matunda hayo.
Aliipongeza Oman kwa
misaada yake mikubnwa inayoendelea kutoa kwa Zanzibar katika Nyanja za
za maendeleo ambayo inazidi kuimarisha uhusiano uliopo kati ya mataifa
hayo mawili.
Naye kwa upande
wake Balozi mdogo wa Oman hapa Zanzibar Bwana Saleh Suleiman Al –Harith
amewapongeza Viongozi na Wananchi wa Zanzibar kwa ushirikiano waliompa
uliomuwezesha kutekeleza majukumu yake vizuri katika kipindi kifupi cha utumishi wake.
Balozi Saleh
alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
kwamba lile ombi la Zanzibar la kutaka mkutano wa ushirikiano wa
wafanyabiashara wa Nchi za Ghuba Oman ikiwa mratibu atalifikisha katika
ngazi zinazohusika wakati ataporejea Nchini mwake.
0 comments:
Post a Comment