Zanzibar. Mojawapo kati ya sababu za kuundwa
kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar ni kumaliza siasa za
uhasama, chuki na kukaribisha siasa za maridhiano, ushindani wa sera na
zenye kutoa majibu ya matatizo ya wananchi.
Kutokana na hali hiyo, vyama vilitarajiwa
vishindane kwenye ulingo sawa wa kisiasa kwa sera nzuri ambazo watu
wataziamini na kuziunga mkono.
Hata hivyo, Zanzibar inakwenda hatua kumi mbele,
inarudi hatua tisa nyuma. hali ya kisiasa hivi sasa inasikitisha na
kukatisha tamaa na iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, inaweza
kuturejesha tena kwenye siasa za chuki na uhasama.
Wanasiasa wanafanya mikutano, wanahuburi chuki,
uhasama, kashfa na ubaguzi, jambo ambalo halioneshi kama kweli kuna nia
safi baada ya maridhiano.
Ninachokiona ni kwamba vyama vya siasa na wanasiasa kwa ujumla wao, hawana jipya la kuwaambia wananchi wa Zanzibar.
Malumbano yanayoendelea ya vyama vikuu kwenye SUK
yanatia kichefuchefu. Zanzibar ina matatizo ya kiuchumi, hali za maisha
ni ngumu, lakini hakuna anayezungumzia masuala hayo zaidi ya matusi na
kashfa.
Wananchi hawana shida ya matusi wala kashfa maana
kama kutukana, kukashfu watu kila mmoja ni mjuzi wa hilo. Watu
wanalotaka ni kuona hali zao za maisha zinakuwa bora zaidi. Wanahitaji
siasa safi na uongozi bora.
Mwishoni mwa Oktoba kuliandaliwa mikutano kadhaa
ya CCM na CUF katika maeneo tofauti ya Unguja na Pemba. Kwenye mikutano
hiyo walihutubia viongozi wenye dhamana kwenye vyama vyao na katika
Serikali.
Ingawa kauli za viongozi hao zinaonekana kuwa
zimejikita kwenye vijembe na vitisho kwa watu wanaotoa maoni
yanayowachukiza wao; wale waliozitamka si watu wapuuzi wala wajinga
wasioelewa uzito na umuhimu wa kuyaenzi maridhiano ya SUK.
Vita hii ya maneno ni uthibitisho wa baadhi ya
viongozi kukosa uvumilivu. Ni dhambi kuruhusu hali hii itawale fikra
zetu. Tutambue kuwa Zanzibar ina matatizo ya kijamii ambayo hayawezi
kutatuliwa kwa ubabe, vitisho wala kuwakashfu watu, bali kwa kuyaenzi na
kuyalinda maridhiano ya kisiasa kwa nia njema.
Ni wajibu wa viongozi kukubali dhamana zao na
wajibu wao mbele ya jamii, pia ni muhimu kwa wanasiasa ndani ya SUK
kuaminiana tofauti na hali ilivyo sasa.
Viongozi katika SUK walio kwenye vyama vya siasa
ni muhimu kutanguliza busara na hekima kuliko jazba na nongwa. Hivyo
basi, CCM na CUF, kama kweli wana dhamira ya dhati kuiepusha nchi yetu
na balaa la kurejea kwenye vurugu na siasa za chuki, hawana budi
wakubaliane kiungwana kuheshimu na kutekeleza maridhiano ya kisiasa.
chanzo;mwananchi.
chanzo;mwananchi.
0 comments:
Post a Comment