Home » » Wahafidhina wawaandama wawakilishi wa CC

Wahafidhina wawaandama wawakilishi wa CC


BAADHI ya viongozi wa CCM wa Zanzibar, vijana na wazee, wananichekesha sana kiasi kwamba nawaona kama watu waliochanganyikiwa ama kutojua hali ilivyo katika dunia ya leo ya utawala wa kidemokrasia.
Kila nikijaribu kutafakari wanayonena, wanayotenda, kauli na vitendo vyao havina lengo jingine lolote lile isipokuwa kutaka wazushe vurugu Visiwani na watu wasielewane.
Wanachokitaka ni kile kinachoitwa patashika nguo chanika, yaani kila penye kheri pawepo shari na kila penye amani pawe na mtihani.
Kwa viongozi wengi wa CCM, hasa wale waliochupia siasa hivi karibui, kaulimbiu ya “Mapinduzi Daima” haimaanishi kutafuta maendeleo, bali ni kuwepo vurugu.
Watu hawa wanafanya kila juhudi za siri na za dhahiri za kuzusha mambo ambayo kama hapatumiki hekima na busara, yanaweza kuzusha tena siasa za chuki na uhasama.
Baada ya kuwasikia baadhi ya hao wanaojiita wastaafu katika Serikali ya Zanzibar na vikosi vya usalama kutaka Unguja na Pemba zitengane na wasiwajibishwe kwa uchochezi wao, sasa tunasikia mengine yasiyokuwa na lengo jingine isipokuwa kupalilia siasa za chuki na uhasama.
Miongoni mwa vichekesho vya vongozi hawa vya hivi karibuni ni kile alichokitoa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Haji Ameir Haji.
Kiongozi huyu, bila ya kutafuna maneno wala kuzungumza kwa mafumbo, amewataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia tiketi ya CCM waache mara moja kuikosoa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika vikao vya Baraza.
Kwake yeye kufanya hivyo ni dhambi kubwa na haisameheki ndani ya CCM. Badala yake anawataka wawakilishi hao siku zote wafanye kila juhudi za kuisifu serikali kwa kutekeleza sera za CCM na ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
Hata pakitokea ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali za serikali, basi wawakilishi wa CCM waisifu serikali, kama matendo hayo ya kihalifu ndiyo sera ya chama hicho.
Kiongozi huyu, bila ya kuona vibaya wala haya, amewataka wawakilishi hao kutofanya urafiki na wala wasishirikiane na wawakilishi wa vyama vingine.
Hapa tujiulize nini lengo la kiongozi huyu katika wakati huu ambao Zanzibar ambayo ilitikisika vibaya kisiasa na watu kutoelewana na hata kuuana ikiwa shuwari na kuanza kujipatia maendeleo.
Kwa kutolewa kauli kama hii, ungelitarajia viongozi wa CCM kumkosoa na hata kumuonya asirudie matamshi kama hayo.
Lakini viongozi wa chama hiki wamekaa kimya, na kitendo hiki ni kielelezo cha utamaduni uliopo ndani ya CCM cha kulindana hata kwa maovu. Hii ni hatari kwa CCM na Zanzibar.
Kukaa kwao kimya kumenipa tafsiri nyingi; mojawapo ni kwamba CCM inazungumzia tu amani na utulivu, lakini vitendo vyake havielekei huko.
Hapa tunapaswa kujiuliza hawa wahafidhina wa CCM wanataka kuipeleka wapi Zanzibar?
Wapo waliotaka Unguja na Pemba zitengane na wakubwa wao kuwavumilia na sasa tunaambiwa wawakilishi wa CCM wasishirikiane kwa njia moja au nyingine na wenzao wa chama cha CUF.
Watu hawa bila ya kuona vibaya wala haya ati wanasema tokea enzi za kale watu wa visiwa hivi sio wamoja. Huu ni unafiki mkubwa.
Wanachojali wao na kuthamini ni karafuu za Wapemba na sio watu wa kisiwa hicho wanaozilima na kuzichuma. Huu ni ubaguzi wa hali ya juu na uchochezi mkubwa wa kisiasa, ambao haufai hata kidogo kulelewa wala kuvumiliwa.
Si ajabu kesho akatokea mtu mwingine katika kundi la wahafidhina akitaka Baraza la Mawaziri la Zanzibar ligawike sehemu mbili, moja ya CCM na nyingine ya CUF.
Baada ya hapo tena akaambiwa Rais Ali Mohamed Shein asishirikiane na wala asishauriane na Makamu wa Pili wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad katika kuiongoza Zanzibar.
Ninaamini kwa dhati kama kauli mbaya kama hii ingelitoka kwa kiongozi wa chama cha upinzani na hasa CUF, basi Zanzibar igekuwa haikaliki.
Tungelisikia watu wengi wanafunguliwa mashitaka ya uchochezi na kuhatarisha amani na utulivu. Lakini kwa vile aliyetoa kauli mbaya kama hii ni kiongozi wa CCM, basi hulindwa kwa nguvu zote kwa vile ni “mwenzetu” na “tumetoka naye mbali”.
Lakini sishangazwi hata kidogo kusikia kauli za hatari kama hizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CCM kwa sababu bado wahafidhina wanaumia ndani kwa ndani kuona Zanzibar imetulia kisiasa na hawafurahii kuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Watu hawa, kwa mujibu wa hali ilivyo, wapo huru kutukana watu matusi ya nguoni hadharani na kuandika matangazo machafu kwenye mbao za maskani zao.
Yote haya yanaonekana hayavunji sheria za nchi kwa vile wanaofanya ni viongozi wa CCM. Kwa maana nyingine ni kusema viongozi wa CCM Zanzibar wapo huru kuvunja sheria na kutoa kauli za matusi na uchochezi.
Sio siri kuwa wengi wa hawa wahafidhina wanadaiwa kuwa ni watu waliozoea kutuma vijana kupiga watu ovyo mitaani na majumbani na kusababisha yatima, vizuka na vilema kwa sababu ya siasa.
Kwa kweli kuwavumilia watu wenye kauli za aina hii, zinazochochea uhasama ni hatari na wanaweza kuwa ndio chanzo cha kuzusha wimbi jingine la vurugu za kisiasa Zanzibar.
Wakati umefika kwa viongozi wa juu wa CCM kutafakari kauli na vitendo vya hawa wahafidhina ambao ninaweza kusema kwa kinywa kipana kuwa hawaitakii mema Zanzibar. Kazi yao kubwa ni fitna tu.
Kuwanyamazia na kutowawajibisha kisheria wale wote wanaotoa kauli za uchochezi au kuhatarisha amani ni jambo la hatari sana. Lazima wawajibishwe kisheria.
Hawa watu hawaitakii mema Zanzibar na watu wake, na kwamba kila mtu muovu ni hatari. Tukumbuke wahenga walivyotuasa kwa kutuambia “majuto mjukuu.”
Jamani wahafidhina ni watu hatari, lakini wahafidhina pia wajue kwamba Wazanzibari wapo macho na hawapo tayari kurejea kwenye siasa za kutukanana, kupigana na kuuana.
Historia katika nchi mbalimbali imeonyesha watu wa aina hii huweza kudanganya watu kwa muda tu na sio siku zote. Mwizi siku zake ni 40, lakini za wachochezi huzidi kidogo tu na haziwi maisha.
Kwa maovu wanayoyatenda na ndoto zao mbaya wanazoitakia Zanzibar, waelewe kuwa wahenga hao hao walitahadharisha watu wabaya kwa kuwaambia; “kila mchimba kisima huingia mwenyewe.”

chanzo;tanzania daima

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa