Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa
Chama hicho katika viwanja vya Fumba, Wilaya ya Magharibi Unguja.
Mwakilishi
wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu (CUF) akiwahutubia wafuasi
na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Fumba, Wilaya ya Magharibi
Unguja.
Mkurugenzi
wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu (CUF) Salim Bimani, akiwahutubia
wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Fumba, Wilaya ya
Magharibi Unguja.
Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi kadi kwa wanachama
wapya 144 waliojiunga na chama hicho huko Fumba, Wilaya ya Magharibi
Unguja. (picha na Salmin Said, OMKR)
Chama
Cha Wananchi CUF kimesema kitaendelea kutekeleza dhamira yake ya
kuwaunganisha wananchi ili kuhakikisha kuwa Wazanzibari wanakuwa kitu
kimoja.
Katibu
Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema iwapo wazanzibari
wataondosha tofauti zao na kusimamia maslahi ya nchi, maendeleo makubwa
yanaweza kupatikana ikiwa ni pamoja na kuwakomboa vijana kutokana na
ukosefu wa ajira.
Maalim
Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Fumba Wilaya ya Magharibi Unguja,
ikiwa ni kuhitimisha ziara yake ya kichama kwa majimbo tisa ya Wilaya
hiyo.
Amesema
kutafuta suluhisho la ukosefu wa ajira kwa vijana ni kipaumbele chake
nambari mbili katika uongozi wake wa kisiasa, baada ya kuwaunganisha
wananchi kuishi kwa umoja na mashirikiano.
Amefahamisha
kuwa zipo njia nyingia za kuwakomboa vijana kutokana na tatizo hilo
ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo ili waweze kuajiriwa katika viwanda
vidogo vidogo na vya kati kupitia kwa wawekezaji wa sekta ya viwanda,
pamoja na kuwaelekeza kujishughulisha na uvuvi wa bahari kuu.
Eneo
jengine alilolitaja kuweza kuwasaidia vijana kuondokana na ukosefu wa
ajira ni sekta ya kilimo ambayo itawasaidia wananchi wengi kwa wakati
mmoja kuondokana na tatizo hilo.
Amefafanua
kuwa kitu cha msingi ni kuwajengea uwezo katika maeneo hayo ili kuweza
kukidhi ushindani wa soko la ajira, sambamba na kuwawezesha kuwekeza
katika kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija zaidi kwa wakulima.
Akizungumzia
kuhusu uhai wa Chama hicho Maalim Seif amesema hali ya chama katika
Wilaya hiyo inaridhisha hasa kutokana na kuendelea vyema kwa chaguzi za
chama katika ngazi za matawi.
Amewataka
wanachama kuwachagua viongozi wazuri watakaoweza kusimamia maslahi ya
chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katika
hatua nyengine Maalim Seif amekemea tabia ya baadhi ya viongozi
kuendeleza chuki na uhasama miongoni mwa wananchi, jambo ambalo amesema
halitoisadia nchi kutimiza malengo yake ya amani na maendeleo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu wa CUF
Salim Bimani, amesema wanakusanya ushahidi wa watu wanaonyimwa haki ya
kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID), ili waupeleke kwa
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.
Amesema
lengo la kukusanya ushahidi huo ni kuthibitisha madai yao kwa Mhe. Rais
kuwa bado baadhi ya wananchi wananyimwa vitambulisho hivyo kinyume na
sheria, ili hatimaye waweze kupatiwa vitambulisho hivyo na kuandikishwa
kuwa wapiga kura.
Nae
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu (CUF) uzalendo wa
kweli unahitajika katika kuondoa kero za kimaisha zinazowakabili vijana
na taifa kwa ujumla.
“Huwezi
kuwa mwana wa nchi ikiwa huna uchungu na nchi yako”, alisema Jussa
akikariri maneno ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume.
Katika
mkutano huo CUF kilivuna wanachama wapya 144, sambamba na kukabidhiwa
kadi 19 kutoka kwa wanachama wa NCCR Mageuzi na kadi 7 kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
0 comments:
Post a Comment