Abdi Omar Maalim, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini, Abdi Omar Maalim, alisema jana kuwa tangu juzi zoezi la uokoaji lilitumia boti nne mbili za wananchi wa Nungwi, moja ya KMKM na nyingine moja ya polisi.
Aliongeza kuwa walikuta baadhi ya mizigo ikielea na kuelekeza kisiwa cha Tumbatu kuendelea na zoezi la kutafuta abiria zaidi.
Maalim aliongeza kuwa baadhi ya wananchi walijitokeza kueleza kuwa hawajawaona jamaa zao na kwamba kwa kutumia takwimu zao na za ofisi yake, hadi jana watu wanane hawakuwa wameonekana.
Jeshi la Polisi Zanzibar limemtia mbaroni nahodha wa boti ya Kilimanjaro ll, Nassor Abubakar Khamis, kufuatia boti hiyo juzi kukumbwa na dhoruba na kusababisha vifo vya watu kadhaa na wengine kuokolewa juzi katika mkondo wa Nungwi.
Alithibitisha kuwa Kapteni Khamis yupo chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Halfan Mohamed Msangi, alipoulizwa kuhusiana na kushikiliwa kwa nahodha huyo, alikataa kutoa maelezo akisema kuwa mwenye mamlaka ya kuzungumzia tukio hilo amepewa kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame. Hata hivyo, Kamishna Makame alipotafutwa jana, simu yake ya kiganjani ilikuwa inaita bila majibu.
Katika hatua nyingine, SMZ juzi usiku ilisitisha kwa muda usafiri wa baharini kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa. Hatua hiyo ilifuatia tukio la boti ya Kilimanjaro ll kupigwa na dhoruba wakati ikitokea Pemba kuelekea Unguja.
Juzi usiku NIPASHE ilishuhudia watu mbalimbali waliokuwa wakitaka kusafiri na boti ya FlyingHorse kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam wakirejea majumbani na mizigo yao na wengine wakisubiri kurejeshewa fedha walizokata tiketi.
Kassim Mbwana, alisema hatua ya kusitishwa huduma za usafiri wa baharini ilimsababishia usumbufu mkubwa katika biashara zake.
Alisema hakukuwa na haja ya kusitishwa kwa usafiri kwani ajali haina kinga muda wowote na popote huweza kutokea.
Ali Muhammed Ali alisema uamuzi uliotolewa na serikali ni mzuri kutokana na hali ya hewa baharini kutishia amani.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment