JESHI la Polisi Zanzibar linamshikilia askari wa Chuo cha Mafunzo
sawa na Magereza kwa Tanzania Bara kwa tuhuma za wizi wa sh 1,635,000
alizoiba kutoka katika duka moja lililopo eneo la Makadara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Mkadam Khamis Mkadam,
alimtaja askari huyo kuwa ni Sajin Meja (S/Sgt) Hassan Iddi Hassan
(45), wa Chuo cha Mafunzo Makao Makuu.
Kamanda Mkadam alisema tukio hilo limetokea jana saa 11 jioni ambapo
askari huyo akiwa amevaa kiraia, alifika dukani hapo kama mteja wa
kawaida wakati muuzaji wa duka hilo akimhudumia mteja mwingine upande
wa pili, askari huyo aliingia ndani na kukimbilia kwenye droo ya pesa
na kuchukua fedha hizo na kuondoka.
“Askari huyo alishuhudiwa na baadhi ya wateja ambao walilazimika
kumshitua muuzaji huyo aliyepiga kelele za mwizi na ndipo alipofukuzwa
na wananchi, na kwa vile eneo hilo lilikuwa karibu na Kituo cha Polisi,
askari waliwahi haraka na kumkamata kabla ya kupata kipigo kikali
kutoka kwa wananchi,” alisema.
Kamanda Mkadam, alisema fedha zote alizoiba mtuhumiwa huyo zimeokolewa, na zimehifadhiwa kama kielelezo mahakamani.
Hilo ni tukio la tatu kutokea Zanzibar katika kipindi cha mwaka huu
ambapo tukio la kwanza ni lile la jaribio la wizi katika maghala ya
Bakhresa eneo la Fuoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo watuhumiwa
watatu walikamatwa wakiwa na silaha aina ya gobore linalotumia risasi
za short gun.
Tukio jingine, majambazi wanne walikamatwa akiwemo Ofisa wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini wakiwa na silaha
tatu zikiwemo bastola mbili na SMG moja baada ya kumvamia
mfanyabiashara na kumpora sh milioni 11.5 eneo la Rahaleo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment