MAKAMU
wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd
amewasihi maofisa maendeleo ya jamii kuhamasisha wananchi kujiunga
kwenye Vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos) wajipatie kipato.
Alisema
hayo juzi jijini hapa wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 50
tangu kilipoanzishwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) Tengeru, sanjari
na mahafali ya tatu ya chuo hicho yaliyotoa wahitimu zaidi ya 109 ambao
walitunukiwa shahada zao na makamu huyo.
Alisema endapo wananchi hawatapewa elimu ya kujiunga na vyama vya kuweka na kukopa, maendeleo hayataweza kupatikana.
Alisema
utoaji wa mbinu za kujikwamua maisha ni muhimu ukatolewa na maofisa hao
ili wananchi waweze kunufaika na mikopo ya chini na ya kati,
inayotolewa katika halmashauri mbalimbali kwa ajili ya kuinua kipato
vyao ndani ya familia.
Alisema
ni fedheha kwa baadhi ya maofisa maendeleo ya jamii kuacha wananchi
wakitaabika wakati wao wanao ujuzi wa kuwezesha kupata mafanikio.
“Naomba
sana maisha ya wananchi yaboreshwe badala ya kuachwa kama hawana watu
wa kuwaongoza, hamasisheni wananchi wajiunge na vicoba kwa maendeleo yao
kwani maofisa maendeleo ya jamii wanapaswa kuwa mfano katika kutetea na
kuleta maendeleo,” alisema.
Wahitimu
109 walitunukiwa shahada ya kwanza ya Maendeleo ya Jamii, Usimamizi wa
Programu za Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Maendeleo pamoja na Stashahada
ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii.
Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba aliwasihi maofisa
maendeleo ya jamii nchini kuhakikisha wanaandaa programu zenye
kuwaletea maendeleo jamii ikiwemo kuwainua zaidi vijana na wanawake
katika kukuza uchumi.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment