Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imemtangaza Mahmoud Thabit Kombo (CCM), kuwa mshindi wa uwakilishi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki uliofanyika jana mjini Zanzibar.
Katika uchaguzi huo, wapiga kura 2,458 ndiyo
waliojitokeza kati ya wapigakura 5,122 walioandikishwa katika Daftari la
Kudumu la Wapiga kura katika jimbo hilo.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi wa
Jimbo la Kiembesamaki, Suluhu Ali Rashid alisema mgombea wa CCM amepata
kura 1,856 sawa na asilimia 76.5 wakati mgombea wa CUF, Abdulmalik Haji
Jecha alipata kura 445 sawa na asilimia 18.3. Mgombea wa ADC Amani
Ismali Rashid alipata kura 84 sawa na asilimia 3.5.
Wagombea wengine na kura zao katika mabano ni
Hashim Juma Issa Chadema (34 sawa na asilimia 1.4), Ali Mohamed Ali wa
Tadea (kura 6 sawa na asilimia 0.2) Ramadhan Simai Mwita akiambulia
kura 1 sawa naasilimia 0.0 kutoka Chama cha Sau.
Suluhu alisema wagombea wa vyama vitano wamesaini
kuyakubali matokeo hayo isipokuwa mgombea wa CUF, Abdulmalik ambaye
aliondoka mapema baada ya matokeo hayo kutangazwa.
“Uchaguzi haukuwa huru na wa haki, kulikuwa na
wizi wa kura, wapo watu walikuwa wakipakiwa kwenye magari na kuletwa
vituoni,” alisema Abdulmalik.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar,
Hamad Mussa Yussuf alisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na hakuna
ukiukwaji wowote wa sheria uliofanyika na kusema ulikuwa ni uchaguzi
mdogo wa mfano kuwahi kufanyika visiwani humu.
Hamad alisema taratibu za uchaguzi ziliheshimiwa
na kufuatwa ikiwa ni pamoja na vifaa kuletwa mapema vituoni huku Daftari
la Wapiga kura likiwa na picha za rangi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Tadea, Ali Juma
Khatib alisema uchaguzi huo ni wa mfano huku akiipongeza ZEC kwa kazi
nzuri ya katika hatua za upigaji wa kura, kuhesabu na majumuisho.
Khatib alisema kimsingi taratibu zote zilifuatwa
katika vituo ikiwa ni pamoja na uchaguzi huo kuwa na uwazi wa kutosha
na matokeo kutangazwa kwa muda mwafaka kwa kutumia teknolojia ya
kisasa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar,
Walide Bakari Jabu alisema matokeo hayo ni fundisho kwa wapinzani na
kusema hizo ni salamu maalumu katika kuelekea mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya
matokeo kutangazwa mshindi mteule wa CCM, Mahmoud Thabit Kombo alisema
atafanya kazi kwa kushirikiana na makundi yote bila ya kujali itikadi za
kisiasa.
“Wakati wa kampeni umemalizika, sasa ni jukumu letu sote kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM na kutimiza ahadi nilizozitoa kwani haziwezi kufikiwa bila ya ushirikiano na kufanya kazi pamoja,” alisema Mahmoud.
Chanzo;Mwananchi
“Wakati wa kampeni umemalizika, sasa ni jukumu letu sote kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM na kutimiza ahadi nilizozitoa kwani haziwezi kufikiwa bila ya ushirikiano na kufanya kazi pamoja,” alisema Mahmoud.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment