Askari Polisi na wafanyakazi wa Kikosi Maalum cha
Kupambana na Dawa za Kulevya, wakiweka viroba vya dawa za kulevya kiasi
cha kilo 201 kwenye mifuko katika Bandari ya Dar es Salaam jana.
Shehena ya dawa hizo ilikamatwa ikiwa kwenye jahazi moja katika Bahari
ya Hindi sehemu ya Tanzania.
Jeshi la Polisi limesema kuwa watu hao walikamatwa na dawa hizo wakiwa katika jahazi.
Kukamatwa kwa kiasi hicho kikubwa cha dawa kuliwashtua baadhi ya wakazi wa wa katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kulazimika kukimbilia katika Bandari ya Dar es Salaam kushuhudia tukio hilo.
Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Wanamaji Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Mboje Kanga, akizungumza na waandishi wa habari jana bandarini jijini Dar es Salaam, alisema raia hao wa kigeni, walikamatwa juzi saa 6:00 usiku wakiwa katika jahazi lijulikanalo kama Aldanial.
Jahazi hilo ambalo linasadikika limetokea nchini Iran, ni mali ya Raisee ambaye ni raia wa nchi hiyo. Hata hivyo, haijafahamika kama dawa hizo za kulevya zilikuwa zikipelekwa wapi.
NIPASHE ilipewa taarifa katika kituo cha polisi kikosi cha wanamaji kuwa waliokamatwa ni Muhamad Hassan (30), Abdul Nabii (30), Fahir Muhamad (34) na Rahim Baksh (30), wote ni raia wa Pakistan.
Raia wa Iran waliokamatwa ni Abdulsamed Badreuse (47), Ayub Hot (50) ambaye ni nahodha wa jahazi hilo, Hazra Azat (60), Nahim Mussa (35), Khalid Ally (35), Kher Muhamad (75), Said Muhamad (34) na Murad Gwaharam (38).
Kamanda Kanga alisema watuhumiwa wote wamewekwa rumande katika Kituo cha Polisi Kikosi cha Wanamaji jijini Dar es Salaam na kwamba uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani haraka wakati wowote.
Aliongeza kuwa ili kubaini dawa hizo ni aina gani, watazipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye pia atabaini thamani yake.
JINSI WALIVYOKAMATWA
Kamanda Kanga alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya Polisi wa Kikosi cha Wanamaji kinachozuia uhalifu baharini kulitilia shaka jahazi hilo na kuanza kulifuatilia.
Alisema polisi walipoanza kulifuatilia jahazi hilo usiku huo, raia wa Pakistan na Iran waliokuwamo ndani yake, walibaini kuwa wanafuatiliwa na walijaribu kukimbia.
Hata hivyo, polisi hao waliokuwa zaidi ya 10 walifanikiwa kuwadhibiti na jahazi hilo pamoja na watuhumiwa kisha likakokotwa hadi katika kituo cha polisi kikosi cha wanamaji na jana asubuhi upekuzi ulianza.
Kamanda Kanga alisema baada ya kufanya upekuzi, walibaini kuwa ndani yake kulikuwa dawa za kulevya kilo 201.
UTATA WA DAWA HIZO
Wananchi waliozungumza na NIPASHE bandarini, walisema kukamatwa kwa dawa hizo kunazua maswali mengi kwa sababu jahazi hilo lilikutwa likiwa limesimama eneo la bahari upande wa Tanzania.
Walishauri kubana watuhumiwa kwani watakuwa wana siri nzito juu ya dawa hizo na kwamba inawezekana kuna watu ambao walikuwa wanawasiliana nao.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment