Tangu kuanzia mwishoni
mwa mwezi Januari, 2014, Zanzibar imeshuhudia mabadiliko ya hali ya hewa.
Mabadiliko ambayo yamekuwa yakiathiri sana miundo mbinu ya umeme katika visiwa
vya Unguja na Pemba.
Hali ya upatikanaji
umeme Zanzibar kwa sasa tokea kuanza kwa mwezi huu wa pili imekuwa siyo ya
kuridhisha katika baadhi ya maeneo. Umekuwepo ukatikaji wa umeme mara kwa mara
hususan katika njia zinazosafirisha umeme kuelekea mashamba kama vile njia ya
Kaskazini, Kusini, Fumba na baadhi ya maeneo ya mjini.
Kuanguka kwa nguzo za
umeme, kupasuka kwa vikombe (pin insulators) katika njia za kusafirisha umeme pamoja
na uchakavu wa miundo mbinu vimekuwa ni sababu kubwa inayopelekea kukatika kwa
umeme mara kwa mara hivi sasa.
Mvua zinazoendelea
kunyesha na upepo unaovuma kwa kasi hupelekea kuanguka kwa nguzo na hatimae
umeme kukosekana. Vilevile, radi zinazopiga huathiri kwa kuunguza vifaa vilivyo katika miundo mbinu ya umeme na
hatimae pia umeme hukosekana.
Hali hii vile vile
inapotokea kwa upande wa Tanzania Bara, husababisha ongezeko la kasi ya umeme
(over voltage) katika njia inayosafirisha umeme kuleta Zanzibar na hupelekea
kisiwa chote kukosa umeme kama ilivyotokea kwa siku ya Ijumaa ya tarehe
14/02/2014 asubuhi na usiku.
Katika kushughulikia
usalama wa miundo mbinu ya umeme, kama vile ubadilishaji wa nguzo mbovu, kila
siku za Alhamisi na Jumamosi, Shirika la Umeme (ZECO) linafanya juhudi za
kubadilisha nguzo hizo ili kumaliza kasoro hiyo katika njia zake za
kusafirishia umeme. Vilevile, juhudi za Shirika zimeelekezwa katika kuzifanyia
matengenezo ya mara kwa mara njia zake za ndani zinazosafirisha umeme ili
kuondokana na kero za kukosekana kwa umeme.
Mwisho, Shirika
linaomba radhi kwa wananchi na wateja wake ambao wamekuwa wakipata usumbufu
kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Aidha, Shirika
linahitaji ushirikiano kutoka kwa wateja na wananchi kwa ujumla kwa kulipatia taarifa Shirika endapo hali yoyote
isiyo salama katika miundo mbinu ya umeme itajitokeza.
Taarifa hizo zitatoa
fursa kwa Shirika kuweza kuchukuwa hatua za kuepesha madhara au kero zinazoweza
kutokea. Vile vile Shirika linatoa wito kwa watu wote kuacha kusogelea au
kugusa nyaya za umeme zilizoanguka chini kwani ni hatari mno.
Kwa kutoa taarifa,
tafadhali piga simu nambari 0242 230 232
Imetolewa na
Shirika la Umeme
Zanzibar
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:
Post a Comment