Home » » TRA mbioni kupiga mnada magogo

TRA mbioni kupiga mnada magogo

  Magogo yakikatwa katika mkoa wa Morogoro, Uvunaji wa miti aina hii umekuwa ukiathiri hali ya hewa hapa nchini

Zanzibar. Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania(TRA)Kanda ya Zanzibar, imesema shehena ya magendo ya magogo yaliyoingizwa Zanzibar kutokea Madagascar yatapigwa mnada au kuharibiwa baada ya Madagascar kutoa ruhusa maalum imeeelezwa jana.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Operesheni wa TRA, Ali Bakari amesema kwamba kikosi kazi maalum cha Taifa cha kupambana na vitendo vya ujangili wa misitu na wanyamapori kimefika Zanzibar kufuatilia suala hilo.
Bakari alisema kikosi kazi hicho tayari kimetupa barua pepe nchini Madagascar kuwataarifu kuhusu kukamatwa kwa mzigo huo na kuwataka kutoa maelezo yakinifu iwapo mzigo huo ulitoka nchini humo na hatua zipi zichululiwe ikiwemo kupigwa mnada au kuharibiwa.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya Utawala wa Forodha ya mwaka 2004, Kamishna wa TRA amepewa uwezo wa kutaifisha mzigo wa magendo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kuupiga mnada na kuutaifisha.
“Tunasubiri majibu ya baruapepe toka nchini Madagascar, hapa kwetu ipo sheria inayotupa uwezo aidha kuupiga mnada mzigo huo, kuuharibu au kuutaifisha kwa mujibu wa sheria,” alisema Bakari.
Alisema kikosi kazi hicho ndicho kilichopokea taarifa ya kuwepo kwa biashara ya magendo ya magogo toka Shirikisho la la Forodha Duniani (WCO) katika kukabiliana na ujangili wa ukataji wa miti adimu katika orodha ya hifadhi ya misitu ya dunia na kufanikiwa kuukamata mzigo huo Zanzibar.
Aidha Bakari alisema iwapo mzigo huo utapigwa mnada, sehemu ya fedha zake zitatumika kulipia gharama katika Bandari ya Zanzibar ambako mzigo huo umekaa kwa kipindi husika chini ya uangalizi wa bandari.
Msimamo huo wa TRA umetolewa siku moja baada ya Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar kueleza kuwa mzigo huo utarudishwa Madagascar.
Chanzo;Mwananchi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa