Home » » Uharibifu mazingira Z`bar wamtisha Maalim Seif

Uharibifu mazingira Z`bar wamtisha Maalim Seif

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar,Maalim Seif Sharif Hamad.
 
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameonya kuwa uharibifu wa mazingira utasababisha athari kubwa ikiwamo kupotea eneo kubwa la ardhi ya Zanzibar
Maalim Seif alitoa onyo hilo jana wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ambayo ardhi yake imezolewa na maji ya Bahari ya Hindi katika kisiwa cha Unguja.

Alisema ili hali hiyo ikomeshwe, viongozi wa mikoa, wilaya na taasisi za serikali zinazohusika na kilimo na mazingira zinapaswa kushirikiana kuielimisha jamii kuacha uharibifu wa mazingira.

Vile vile, alisema viongozi hao wanatakiwa kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wote watakaobainika kuharibu  mazingira.

Akiwa katika ziara hiyo, Maalim Seif alijionea ukuta uliojengwa na mwananchi mmoja katika eneo la ufukwe wa bahari hiyo ya Mkokotoni juu ya bomba linalopeleka maji katika kisiwa cha Tumbatu na kuagiza uvunjwe kwa gharama zake.

Maeneo mengine aliyoyatembelea ni ya Kilimani, Mnazi Mmoja, Kisakasaka Mkoa wa Mjini Magharibi na Pete na Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja.

Maeneo hayo ni miongoni mwa 148 ya Unguja na Pemba ambayo  yamekumbwa na athari kubwa kutokana na uvamizi wa maji ya bahari kulikosababishwa na shughuli za kibinadamu.

Baadhi ya shughuli hizo ni pamoja na ukataji mikoko, uchimbaji mchanga, uvuvi haramu na athari za mabadiliko ya tabianchi.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa