Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Suala la uwiano wa wajumbe katika Bunge Maalumu la Katiba, kati
ya Tanzania Bara na Zanzibar, juzi jioni lilizua malumbano yaliyotokana
na mjumbe, Said Ally Mborouk, kueleza kuwa Zanzibar kwa muda mrefu
imekuwa ikionewa na kudhulumiwa.
Hali hiyo ilijitokeza wakati wajumbe hao
walipokuwa wakichangia michango yao katika Rasimu ya Kanuni ya
Uendeshaji wa Bunge hilo mjini Dodoma.
Mbarouk alisema Zanzibar ni moja ya nchi mbili
zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba kuna haja ya
kuitendea haki kwa kuhakikisha kuwa inakuwa na idadi sawa ya wajumbe
wakati Bunge litakapoanza vikao.
“Sisi Wazanzibari kwa muda mrefu tumekuwa
tukilalamika kuwa Watanganyika wamekuwa wanatuonea, wanatudhulumu katika
Muungano huu. Mara nyingine mjadala wa malalamiko haya hufanyika katika
Baraza la Wawakilishi ambalo wewe mheshimiwa Mwenyekiti (Pandu Ameir
Kificho) ni Spika,” alisema na kuongeza;
“Sasa wenzangu wa Zanzibar tumepata nafasi kwa
kushirikiana na wenzetu wa Tanganyika ama kuimarisha au kuusambaratisha
Muungano wetu.”
Alisema utungaji wa kanuni hizo unaweza kuzaa
katiba itakayosaidia kuondoa uonevu, dhuluma na kero za Muungano
zilizodumu kwa miaka 50 iliyopita.
Pia alisema kanuni hizo zinaweza kuzaa Katiba
itakayoendeleza kero ama kusambaratisha kabisa Muungano kama ambavyo
imetokea kwenye nchi nyingine duniani zilizokuwa zimeungana.
Alisema Bunge hilo lina nafasi kubwa ya kuondoa
kero za Muungano na kwamba ni lazima suala hilo lianzie katika utungaji
wa kanuni.
Kauli hiyo ilimfanya Job Ndugai ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kusimama na kujibu.
Katika majibu yake, Ndugai alisema kuna muhimu wa
wajumbe kuwa na umakini katika lugha wanazozitumia katika vikao vikubwa
kama hicho.
“Lugha ni muhimu sana. Utu wa mtu uko katika
lugha... kitu muhimu ni kujenga hoja ili wenzako wakuunge mkono,”
alisema na kuongeza: “Lakini anaposimama mtu akasema kwa miaka 50 ya
Muungano huu kumekuwa na dhuluma na uonevu na mambo kama hayo ehh, haya
bwana.”
Alisema Bunge hilo ndio mahali ambapo watu wanaweza kutoa madukuduku yao lakini kwa kutumia lugha za kistaarabu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment