Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ifikapo mwaka 2015 hamasa za kisiasa kwa upande
wa Zanzibar zitakuwa katika kiwango cha juu huku ikitegemewa kutokea
kwa mabadiliko ya uamuzi miongoni mwa wapigakura, hususan vijana ambao
wengi wao wamezaliwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Mabadiliko yatajitokeza kuanzia wakati wa
kutafuta wagombea kupitia vyama vya siasa na katika hatua hii, makundi
ya vijana yatajiunga pamoja kuona wanafanikiwa kupenyeza watu wao,
lakini pia yale mambo ambayo wanadhani yatawafikisha katika maisha bora
zaidi watayapa nguvu huku wakiwapuuza wanasiasa ucharwana wababaishaji
wengine.
Vijana wengi wanaonekana kuanza kuzitupia kisogo
siasa zisizowahakikishia maisha bora, Si vyama vya upinzani au vyama
tawala; vyote vitakuwa katika wakati mgumu kipindi hicho.
Lakini ugumu zaidi utajitokeza ikiwa atajitokeza mwanasiasa mwenye kubeba matumaini ya vijana baada ya uchaguzi.
Zile porojo za mifereji kutoa maziwa na asali
naona hazitasikilizwa tena na kundi la vijana ambao wengi wao wamekata
tamaa, hasa wakitazama siku zinakwenda huku ahadi za wanasiasa ni zile
zile hakuna jipya, hazibadiliki wakati mambo yamebadilika.
Jambo moja ambalo kwa upande wa Zanzibar vyama
vya siasa vinapaswa kushukuru Mungu ni kitendo cha Katiba kukubali
kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo inavihakikishia
vyama vyote vitakavyoungwa mkono na wapigakura kwa asilimia kubwa kuwemo
ndani ya serikali.
Kwa hali ya mambo inavyokwenda, mabadiliko ya
wapigakura, mabadiliko ya kiuchumi duniani, ukosefu wa ajira na
kuongezeka kwa tofauti kubwa kati ya walionacho na wasionacho, hakuna
chama cha siasa kitakachoweza kutamba kuwa kina uhakika na ushindi.
Wale wanaomkejeli rais wa awamu ya sita,
Zanzibar, Amani Abeid Karume kwa kitendo chake cha kukubali mabadiliko
katika mfumo wa siasa wakati wa uongozi wake, wataweza kujutia vitendo
vyao pale matokeo ya uchaguzi yatakapotangazwa huku vyama karibu vyote
vilivyoshiriki uchaguzi vikikaribiana sana.
Ingawa hilo siyo jambo geni katika historia ya
siasa za Zanzibar, lakini katika hali ambayo haitotarajiwa, karata ya
mwisho ya kuamua mshindi katika uchaguzi mkuu ujao, itachezwa na
wapigakura vijana ambao watatazama zaidi namna wanavyoweza kuvuka katika
dimbwi la umaskini.
Wakati wa viongozi wenye sifa za shaka shaka
umeshapita, wenye visasi na kukurupuka katika utendaji kwa maslahi
binafsi umeshapita ni zama za siasa za maridhiano huku siasa ikitumikia
uchumi na kuonekana kwa vitendo kubadilika kwa maisha ya watu na sio
ukuaji wa uchumi kwa takwimu za vitabuni.
Jambo hili siyo la kufikirika, ni suala lililo
wazi kabisa kwamba vijana watatumika kama nguvu kubwa ya mageuzi ya
kisiasa, kijamii na kiuchumi na hali hii sio kwa Zanzibar tu, bali
litazikumba nchi karibu zote Afrika.
Wazanzibari walio chini ya miaka 30 wanawakilisha
zaidi ya asilimia 78 ya idadi ya watu, hivyo vijana wengi wanaonekana
kama vile kukatishwa tamaa na vikwazo vya kielimu, ajira na masuala
mengine katika jamii ndani ya ulingo wa kisiasa na nje pia.
Taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kwamba asilimia 78 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 35 na nusu yao wapo chini ya umri wa miaka 17.
Taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kwamba asilimia 78 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 35 na nusu yao wapo chini ya umri wa miaka 17.
Hawa ni vijana ambao wanataka kuona matumaini yao yakitimia katika maisha.
Lazima tukubali kwamba matumaini ya vijana
yanajengwa kwa uhalisia wa mambo na kwamba masuala ya kuboresha huduma
za kijamii za elimu, makazi bora, afya, maji safi na salama, demokrasia
na utawala bora ni mambo ambayo vijana wanayatizama kwa jicho pana.
Katika kufikia kutimiza haja za vijana tunahitaji
kufikiria zaidi mfumo bora na imara wa mundo Muungano wetu ambao
utawahakikishia fursa za ajira na kupunguza umaskini kwa kiwango
kikubwa.
Jamii ya vijana katika nchi inatazamwa kwa
umakini zaidi hasa kwa sababu ya nguvu za ushawishi kisiasa, kiuchumi
na hata kijamii.
Katika uchaguzi mkuu hapo mwakani, vijana wa
Zanzibar wanasema watakachohitaji ni hatma yao watawezaje kumudu hali za
maisha katika changamoto ya ukosefu wa ajira na udhaifu wa maamuzi ya
watekelezaji sera?
Wakati hayo yakiendelea kwa wapigakura vijana,
kwa wanasiasa nako hali itakuwa ngumu zaidi kwao maana kwa kipindi
kirefu sasa wametoa msukumo kidogo kwa kipaumbele cha kuondoa umaskini,
maisha bora,lakini pia hakuonekani kama kuna dhamira ya dhati ya
kukwamuka, hivyo wapigakura vijana wasiokuwa na ajira, makazi bora
wanaweza kuvutiwa na mwanasiasa atakayewapa matumaini yanayoingia
akilini mwao.
Uchaguzi wa mwakani utakuwa ni wa tano tangu kurejeshwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Bila shaka kutakuwa na mabadiliko ya kila aina,
kuanzia wagombea, kampeni na hata aina ya hotuba za mikutano ya kampeni
inategemewa kuywa tofauti sana na chaguzi zilizopita.
Wapigakura waliozaliwa mwaka 1992 ambao mwakani
watakuwa ni sehemu ya wapigakura katika uchaguzi mkuu, watakuwa
wameshapata picha ya wanasiasa tulionao.
Siyo wadogo tena wa kuweza kuwabaini wanasiasa
wababaishaji, wazugaji na wasaka tonge kwani vijana wamejifunza mengi,
wameyaona mengi, wamewajuwa wanafiki na watu wakweli, wamewaona
wababaishaji na watu makini.
Hawatafanya uzembe tena, watakuwa makini kupembuwa
mchele upi na pumba zipi, nani msakatonge na nani anawafaa kwa
kubadilisha maisha yao, nani atawapa shibe ya siku moja katika maisha ya
miaka mitano ijayo na nani atawapa neema ya maisha yaliotononeka
angalau kuvuka mstari mwekundu wa umaskini.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment