Home » » MBOWE:NITATANGAZA KUTETEA KITI CHANGU CHADEMA MUDA UKIWADIA

MBOWE:NITATANGAZA KUTETEA KITI CHANGU CHADEMA MUDA UKIWADIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe.
Wakati fomu za kuomba kuwania uenyekiti na makamu wake Tanzania Bara na Zanzibar wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zikianza kutolewa leo, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, amesema atatoa taarifa iwapo atatetea nafasi yake au la kama atachukua fomu hizo muda wa kufanya hivyo utakapowadia.
Mbowe alisema hayo alipozungumza na NIPASHE jana, kujua iwapo atatetea nafasi yake au la katika uchaguzi mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Septemba 14, mwaka huu.

“Muda wa kuchukua fomu ukiwadia nitatoa taarifa,” alisema Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumzia utaratibu, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uratibu wa Kanda wa Chadema, Benson Kigaila, alisema fomu za kugombea nafasi hizo kubwa ngazi ya taifa ndani ya chama hicho zinaanza kutolewa leo.

Kwa mujibu wa Kigaila, fomu hizo zinapatikana katika ofisi za Chadema zilizopo nchini kote na kwenye tovuti ya chama hicho.

Alitaja nafasi zinazogombaniwa kuwa ni ya mwenyekiti wa Taifa na Makamu wake kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema baada ya wanachama wanaotaka kugombea nafasi hizo kujaza fomu hizo, wanapaswa kuzirudisha kwa ofisi ya katibu makao makuu ya chama hicho.

Kuhusu ngazi nyingine za uongozi, zikiwamo za mabaraza, alisema fomu zake zilianza kutolewa tangu Agosti 10, mwaka huu.

Akizungumza hivi karibuni kuhusu uchaguzi mkuu kwa ngazi hiyo, ambao unatarajiwa kufanyika mwezi ujao, Kigaila alisema nafasi zote zipo huru hata kwa viongozi wa ngazi hizo.

Alisema viongozi hao ni waliopo sasa madarakani tofauti na kauli iliyotolewa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwamba hawapaswi kugombea tena kwa mujibu wa sheria ya katiba ya chama hicho.

Uchaguzi huo pia utahusisha viongozi wa mabaraza ya chama hicho ambayo ni pamoja na Baraza la Vijana (Bavicha), Wazee na Wanawake (Bawacha) ambalo uchaguzi wake utafanyika Septemba 11 mwaka huu.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa