Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kocha wa Simba, Patrick Phiri amepatwa na kigugumizi cha uamuzi
wa nani abaki kati ya Mkenya Donald Mosoti na Mrundi Butoyi Hussein
kujaza nafasi ya beki wa kati.
Hadi jana, Phiri alikuwa akikuna kichwa kuhusu nani asajiliwe msimu ujao baina ya wachezaji hao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Phiri alisema
wachezaji wote ni wazuri, lakini anahitaji muda zaidi wa kufanya uamuzi
wa busara.
“Natakiwa kuwa makini katika uamuzi wangu kuhusu nani nimchukue kati ya Mosoti na Butoyi.
“Nimewaona katika mazoezi, Mosoti ni beki mzuri
hata huyu mpya (Butoyi), pia ni mzuri, ila nitaendelea kumwangalia
zaidi,” alisema.
Wiki hii, uongozi wa klabu ya Simba ulimleta
nchini kwa majaribio beki huyo mpya kutoka Telecom ya Djibouti ambaye
kwa Kirundi jina lake lina maana ya Dotto. Butoyi alianza mazoezi na
Simba juzi huku Zacharia Hanspoppe akiwa na matumaini kuwa ndiye
atakayechukua nafasi ya Mosoti.
Mosoti alisema hata ikitokea akaondoka Simba kabla
ya Desemba kama walivyokubaliana haitakuwa tatizo kwani ni mpango ambao
upo, ingawa alipendelea kuachana na timu hiyo wakati wa dirisha dogo la
usajili.
Awali, Mosoti aliomba kuvunja mkataba na Simba ili
ajiunge na klabu moja ya nchini Qatar ambayo alikwenda kufanya
majaribio na kufuzu. Hata hivyo ilishindikana kutokana na kuwa na
mkataba mrefu.
“Nilizungumza na waajiri wangu (Simba) kuhusu hilo, walinikubalia kuwa nikitaka kuondoka nitaruhusiwa.
Baada ya mazungumzo niliona ni vyema niondoke
Desemba, ila kulikuwepo na makubaliano kwamba ikitokea hata kabla ya
wakati huo niruhusiwe, hivyo hakuna tatizo kwa hilo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Phiri amesema anaanza
kukipima kikosi chake kwa kucheza mechi na timu ndogo kabla ya kuangalia
michezo ya kimataifa.
Simba ipo visiwani hapa inafanya mazoezi yake
kwenye uwanja wa Chuoni na keshokutwa usiku itacheza mechi yake ya
kwanza ya kirafiki na timu ya daraja la pili ya Kilimani City. Mechi
hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Amaan
Mbali na mchezo huo wa kwanza kwa kocha huyo Mzambia, Simba pia
itacheza na Miembeni inayoshiriki Ligi Kuu ya hapa wiki ijayo, Tanzania
Prisons na Mtibwa Sugar ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara.
Phiri alisema kuwa wachezaji wake wanatia moyo
kwani wameonyesha mabadiliko makubwa na hakusita kumsifu beki wa kulia
wa timu hiyo, Nassoro Masoud ‘Chollo’ akisema kuwa kiwango chake
kimepanda.
Msimu uliopita Chollo alitumia muda mwingi nje ya
uwanja kutokana na kuwa majeruhi na hivyo kutoa nafasi kwa beki
chipukizi, William Lucian ‘Gallas’ kucheza nafasi yake.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment