Home » » TAN TRADE YAPONGEZWA KWA KUZINGATIA USAWA

TAN TRADE YAPONGEZWA KWA KUZINGATIA USAWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

WAZIRI wa Viwanda, Masoko na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bw. Nassor Ahmed Mazrui, ameipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kwa kuwa na utendaji unaozingatia usawa kati ya Bara na Zanzibar kwa kuboresha biashara pande zote.

Bw. Mazrui aliyasema hayo katika hafla ya Uzinduzi wa Maonesho ya Biashara ya Idi el Fitri yanayofanyika kwa siku nane visiwani humo.

"Mimi kama waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya masoko, viwanda na biashara katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nimeshuhudia utendaji mzuri ndani ya TanTrade unaozingatia usawa wa kibiashara kati ya Bara na Visiwani.

"Kupitia Tan Trade, wafanyabiashara wa Zanzibar wanapata fursa ya kushiriki katika maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ambayo yanaandaliwa na Mamlaka hii bila kujali upande ambao maonesho haya yanaandaliwa...hili ni jambo jema la kupongezwa kwani linakuza uchumi wa nchi na kutoa fursa sawa kwa wafanyabiashara," alisema Bw. Mazrui.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani, kuboresha bidhaa zao na kutumia fursa wanayoipata katika maonesho mbalimbali wanayoshiriki kwa kujenga mahusiano ya kibiashara na mtandao ambao utaweza kuwaongezea mauzo ndani na nje ya nchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TanTrade, Sabetha Mwambenja alisema mamlaka hiyo itaendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara wa Tanzania na kuhakikisha ubora na viwango vya bidhaa nchini unaboresheka.

Alisema mamlaka hiyo iko katika hatua za mwisho kukamilisha ofisi za kuduma visiwani Zanzibar.

"Tunatambua umuhimu wa kuboresha na kupanua huduma zetu hivyo tuliiomba Serikali itusaidie kupata jengo ambalo tutaweza kulitumia kama ofisi za kudumu na tukapatiwa jengo hilo, hivi sasa tuko katika hatua za mwisho kukamilisha ofisi zetu visiwani Zanzibar.

"Naipongeza Serikali kwa namna inavyounga mkono jitihada zetu za kukuza biashara na uchumi wa Taifa, tunawaahidi wafanyabiashara wote na Watanzania kuwa, TanTrade tutasimamia na kutoa fursa sawa kadri inavyowezekana," alisema.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade, Bi. Anna Bulondo, alitoa wito kwa taasisi za Serikali, Mashirika binafsi na Jumuiya za wafanyabiashara, kufanya maandalizi ya Maonesho ya Mapinduzi ya Zanzibar mapema ambayo yatafanyika kwa mara ya pili Mjini Zanzibar.

"Naomba kutoa wito kwa taasisi mbalimbali za Serikali, Mashirika binafsi na wafanyabiashara, kufanya maandalizi mapema ya maonesho ya Mapinduzi ambayo yatafanyika kwa mara ya pili hapa visiwani baada ya kufanyika kwa mafanikio makubwa mwaka 2013 wakati wa sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar," alisema

 Chanzo;Majira

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa