Home » » KINANA APOKELEWA KWA MABANGO

KINANA APOKELEWA KWA MABANGO

 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amejikuta akipokelewa kwa mabango na wananchi na kulazimika kuwaagiza viongozi wa chama hicho Mkoa wa Kusini Unguja, na ofisi kuu CCM kusuluhisha mgogoro uliopo kati ya mbunge na mwakilishi wa jimbo la Uzini.

Akizungumza baada ya kushiriki kazi za ujenzi wa tawi la CCM Miwani, Kinana alisema kutokuwapo kwa maelewano kati ya viongozi hao, kunatishia kukiangusha chama hicho kwa kushindwa kuwapelekea maendeleo wananchi.

Kinana alilazimika kutoa agizo hilo bada ya wananchi wa Miwani na vijiji jirani kumkaribisha kwa kubeba mabango yaliyokuwa na ujumbe kadhaa ukiwamo uliosomeka “Mbunge na Mwakilishi jimbo la Uzini hawaelewani”.

Bango lingine lililalamikia wananchi hao kutokupata huduma muhimu za kijamii kama afya, maji na miundo mbinu ya barabara.

Mbunge wa Uzini ni Dk. Mohamed Seif Khatibu na Mwakilishi ni Mohamed Raza.

Aidha, amewataka wanachama wa CCM kuwa na umoja na mshikamano, na kutokubali kugaiwa makundi.

Aliwahakikishia wana-CCM wa Mkoa wa Kusini Unguja, wakiwamo wananchi wa Miwani kuwa malalamiko yao atayafikisha kwa Mwenyekiti wa Chama, Rais Jakaya Kikwete, ili yatafutiwe ufumbuzi, ukiwamo ubovu wa barabara.

 Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema baada ya kumalizika kwa ziara ya Kinana, CCM Zanzibar watafanya tathmini majimbo ambayo yana migogoro na yanaathiri utekelezaji wa Ilani yake na hatua zitachukuwa dhidi ya viongozi wa jimbo ambao hawana maelewano.

 “Kama inafikia hatua mpaka wananchi wanabeba mabango kutokana na kutoelewana kwa mbunge na mwakilishi kweli tatizo hilo lipo na hatuwezi kulifumbia macho na naahidi tutalishughulikia,” alisema Nape.

 Dk. Khatibu alisema wananchi hao walitumia demokrasia, ingawa alisema hawakupaswa kumeonyesha mabango Katibu Mkuu. Raza hakupatikana kutokana na kuwa safarini nje ya nchi.
 
SOURCE: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa