Kocha mkuu wa Simba, Goran Kopunovic (wa pili kushoto) kitoa maelekezo
kwa baadhi ya wachezaji katika mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika
kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislamu Chukwani, kujiandaa na mchezo wao wa
leo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Polisi Zanzibar. Kulia ni kocha
msaidizi, Seleman Matola
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanaingia katika hatua ya nusu
fainali hii leo, wakati timu mbili kutoka Tanzania Bara, Simba na Mtibwa
Sugar zitakapocheza dhidi ya mbili za visiwani Zanzibar, Polisi
Zanzibar na JKU (Jeshi la Kujenga Uchumi)
Simba ilifuzu kwa hatua hiyo baada ya kuifumua
Taifa Jang’ombe kwa mabao 4-0 na leo inakutana na Mafunzo katika mchezo
wa nusu fainali.
Kwa upande wao, Mtibwa ilifanikiwa kutinga nusu
fainali baada ya ushindi wao wa mikwaju ya penalti dhidi ya Azam FC,
zilipomaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1 juzi.
JKU iliwashangaza wengi kwa kuwaondoa mabingwa wa
zamani wa Tanzania Bara walioanza mashindano hayo kwa kasi kubwa, Yanga,
licha ya kushambuliwa muda mwingi wa mchezo huo kabla ya kuibuka na
ushindi wa bao 1-0 juzi.
Mchezo wa kwanza wa leo utakaozikutanisha Mtibwa
dhidi ya JKU unatazamwa kwa tofauti kubwa hasa kutokana na maafande hao
wa visiwani kuishangaza Yanga kwa bao la kushtukiza na kulilinda muda
wote wa mchezo. Tangu kutua kwa kocha huyo raia wa Serbia, Simba
imeimarika kwa kushinda mechi zote tatu ilizocheza baada ya kupoteza
mechi ya ufunguzi na itaingia katika mchezo wa leo ikiwa na tahadhari
kubwa kutokana na timu za Zanzibar kutotabirika.
Akizungumzia mchezo huo, Kopunovic alisema
kutokana na matokeo yaliyomshtua ya vigogo Yanga na Azam kutolewa juzi
katika mechi zao za robo fainali, wamejipanga kuhakikisha wanaitumia
hali hiyo kama tahadhari kwao kwani Polisi pia waliwavua ubingwa
mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda.
“Hakuna aliyeweza kufikiria kwa haraka kitu kama
kile cha Yanga na Azam kutolewa mapema, hata mimi nimeshtuka, hii
inathibitisha kwamba kuna timu hazitabiriki, sasa akili yetu ni kwamba
tunataka ushindi lakini ni lazima tuongeze umakini katika uchezaji
wetu,” alisema Kopunovic
Wakati Kopunovic akisema hivyo, kocha mwenzake wa
Polisi, Hamis Sufiani alisema baada ya kuiondoa KCCA sasa wanataka
kufanya kama hivyo kwa Simba kutokana na kuwa na uwezo wa kuwafunga
wekundu hao.
“Kwetu mechi ngumu ilikuwa ni ile dhidi ya KCCA
ambayo kwanza inatoka nje, lakini aina ya soka lao tulikuwa hatulijui,
sasa tunakutana na Simba ambayo tunaijua karibu kila kitu, tunataka
kuifunga ili tulibakishe kombe hili hapa kwetu,” alitamba Sufiani.
Mchezo wa mapema utakaopigwa jioni utazikutanisha
Mtibwa Sugar ya Morogoro itakayoumana na JKU katika mchezo ambao utakuwa
ni kusaka mshindi mara mbili kutokana na timu hizo kutoka kundi moja
huku zote zikitoka sare ya kufungana bao 1-1.
JKU iliyokata tiketi hiyo kwa kuifunga Yanga bao
1-0 itakutana na Mtibwa Sugar ambao iliwaondoa matajiri wa Azam kwa
mikwaju ya penalti 7-6.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Mtibwa, Mecky
Mexime alisema wamejiandaa vizuri kupata ushindi katika mechi hiyo
ambayo wanatambua kwamba wanakutana na timu ngumu.
Wanajeshi hao wa JKU ni wazi wataingia katika mchezo huo wakijivunia kasi ya mshambuliaji wao maarufu Amour Mohamed ‘Janja’.
Chanzo:Mwananchi
Wanajeshi hao wa JKU ni wazi wataingia katika mchezo huo wakijivunia kasi ya mshambuliaji wao maarufu Amour Mohamed ‘Janja’.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment