Chini ya Serikali ya awamu kwanza kulikuwa na kasi ya ujenzi wa viwanda,
karakana, mashirika ya Serikali. Usafirishaji wa mazao kama pilipili,
mbata na karafuu nao ulikuwa juu na kuiwezesha Zanzibar kupata fedha za
kigeni hatua iliyosaidia kuimarisha uchumi
Zanzibar ya Karume
Chini ya uongozi wa Karume, Zanzibar inatajwa kama
nchi iliyokuwa ikipiga hatua nzuri hasa katika maendeleo ya uchumi
kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.
Kwa mfano, ‘tarikhi’ ya Zanzibar inaonyesha
wananchi walikuwa wakipata huduma za maji safi na salama, afya, chanjo
na matibabu, kujengewa makazi bora na ya kisasa.
Chini ya Serikali ya awamu kwanza kulikuwa na kasi
ya ujenzi wa viwanda, karakana, mashirika ya Serikali. Usafirishaji wa
mazao kama pilipili, mbata na karafuu nao ulikuwa juu na kuiwezesha
Zanzibar kupata fedha za kigeni hatua iliyosaidia kuimarisha uchumi.
Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kuwa msingi wa
Mapinduzi ulikuwa ni kuwatoa wananchi katika kadhia ya unyonge, uonevu,
ukandamizaji wa haki na fursa. Pia kuwapatia huduma bora za jamii baada
ya kuondoa utawala wa Kisultan uliohamia kutoka Oman.
Baada ya Mapinduzi, ujenzi wa viwanda vya sigara,
mvinyo, nguo, sukari, soda, viatu, maziwa, magodoro na vitu vya
nyumbani, kulitanua wigo wa ajira kwa wananchi, huku kukiwa na kasi
kubwa ya uzalishaji mazao shambani kutokana na Serikali kupeleka
pembejeo na mbolea kwa wakulima.
Hali ilivyo sasa
Kati ya mambo yaliyowasukuma Waafrika wa Zanzibar
na kulazimika kukiunga mkono Chama cha Afro Shirazi Party ( ASP) ilikuwa
ni tatizo la ardhi. Walowezi na mabebari wengi ndiyo waliokuwa
wakimiliki na kuhodhi ardhi yenye rutuba.
Awamu ya kwanza iligawa ardhi kwa wananchi, lakini hali ilivyo sasa ni sawa na ile iliyokuwa kabla ya Mapinduzi mwaka 2964.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega
uchumi Zanzibar (ZIPA), Nassor Salum anasema hivi sasa Zanzibar
inakabiliwa na tatizo kubwa la uwekezaji wa miradi hasa katika sekta ya
utalii, kutokana na maeneo mengi ya fukwe hasa katika ukanda wa
Mashariki kuchukuliwa na baadhi ya vigogo na watendaji serikalini.
“Maeneo makubwa ya ardhi yamehodhiwa, kuzungushwa
kuta bila ya kuendelezwa kwa maelezo kuwa yamekuwa yakiwekwa ili
kusubiri matajiri wa nje na ndani na kuuzwa kwa bei ya juu,’’ anasema.
Elimu
Wakoloni walitoa elimu kwa misingi ya rangi,
Waafrika waliwekwa kando. Miaka 51 ya mapinduzi wananchi hawaridhiki na
hali ilivyo kwenye sekta hiyo.
Ukweli ni kuwa elimu Zanzibar inaendeshwa
kimatabaka. Wananchi walio wengi wanasomesha watoto wao katika shule za
Serikali zinazokabiliwa na changamoto nyingi za kitaaluma. Watoto wa
viongozi, matajiri wengi wanasoma shule binafsi zenye mazingira bora ya
utoaji taaluma.
Makazi
Kabla ya mapinduzi, nyumba nyingi za wananchi
wenye asili ya Kiafrika, zilikuwa zikisikitisha. Zilijengwa kwa miti,
udongo na kuezekwa kwa makuti au vipande vya madebe.
Hali hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu
zilizowahamasisha wananchi kukiunga mkono Chama cha ASP, kilichofanikiwa
kuuondosha utawala wa Kisultan uliokuwa ukilindwa na Waingereza.
Hata hivyo, mara baada ya Mapinduzi, Serikali ya
awamu ya kwanza, ilitimiza ahadi ya kuwapatia wananchi makazi bora kwa
kuwajengea makazi bora. Mpango huo uliendelezwa na awamu zilizofuatia
ingawa haukuwa na tija kubwa kwa wananchi wanyonge, kutokana na nyumba
nyingi za gharama nafuu zilizojengwa kuhodhiwa na vigogo badala ya
wananchi makabwela.
Kilimo
Wananchi wanyonge kabla ya Mapinduzi walipata
dhiki katika ufanyaji wa kazi za kilimo kutokana na ardhi kubwa
kuhodhiwa na walowezi na matajiri.
Wengi walilazimika kukodi ardhi kwa ajili ya kilimo na sehemu ya mazao waliopata walitakiwa kuwapa waliowakodisha ardhi.
Yalikuwa ni madhila na mashaka makubwa
yaliowakumba Waafrika. Mara baada ya Mapinduzi, Serikali iliwapa ekari
tatu kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo.
Hata hivyo, leo kilimo kimedorora licha ya kuwa
sehemu kubwa ya visiwa vya Unguja na Pemba kuna ardhi ya kutosha yenye
rutuba. Kilimo hicho kwa sasa kinachangia asilimia 31 ya pato la
Zanzibar.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo,
Serikali imekuwa ikitenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya bajeti ya
mishahara badala ya bajeti ya miradi ya maendeleo.
Taarifa zinaonyesha bajeti ya mwaka inayokwenda
katika mishahara ni zaidi ya Sh12 bilioni, ilhali bajeti inayotengwa kwa
maendeleo ni Sh1.5 bilioni. Kinachosikitisha ni kuwa wahisani ndio
wanaoonekana kuwa na uchungu na kilimo kwa kutenga bajeti ya Sh8 bilioni
kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Afya
Mchango wa Serikali katika kutoa huduma za afya
baada ya miaka 51 ya Mapinduzi, hauridhishi hali inayosababisha Wizara
ya Afya kuonekana ni tegemezi kwa wahisani.
Kwa sababu ya udogo wa bajeti ya sekta ya afya,
huduma nyingi zimezorota, huku idadi ya wagonjwa wanaolazimika kutibiwa
nje ikiongezeka kila mwaka. Fedha nyingi zinatumika nje kwa ajili ya
kuwatibia wagonjwa wa moyo na saratani, kwa kuwa nchi haina wataalamu
bingwa wa magonjwa hayo na vifaa vya kisasa.
Tunatekelezaje malengo ya Mapinduzi?
Ili Serikali ionekane ikitekeleza malengo ya Mapinduzi, haina budi kusimamia dhana ya usawa, haki na uwajibikaji.
Kero tete za wananchi kama vile kushamiri kwa rushwa, kuuzwa kwa
ardhi, elimu duni, huduma mbaya za afya, zinaweza kufikia kikomo ikiwa
Serikali itaamua kuzifungia kibwebwe.
Kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na hata Taifa, hatuna budi kuwekeza katika elimu, kilimo, ufugaji, uvuvi na ujenzi wa viwanda.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment