Mwaka jana tulishuhudia kituo kikubwa cha habari duniani
kikiyataja matamasha saba bora ya kimataifa na Sauti za Busara likiwa
tamasha lililoshika nafasi ya tatu.
Ni tamasha ambalo watu kutoka katika pembe zote za
dunia, wiki ya pili ya Februari kila mwaka hukutana katika kisiwa cha
marashi ya karafuu, Zanzibar ambako ndiko tamasha linakofanyika.
Kipindi cha Februari, Zanzibar ni eneo
linalochangamka, eneo hilo lenye majengo ya kale hupambwa na muziki wa
kisasa wa Kiafrika.
Watalii, wazawa, wanamuziki wakubwa wanaoimba na
kupiga ala za muziki hukutana sehemu yenye mandhali iliyotulia, ndani ya
eneo lenye hazina yenye historia na iliyo bora katika Afrika Mashariki
Mji Mkongwe, Zanzibar pembezoni mwa Bahari ya Hindi ili kuchota sauti
zenye busara zinazozalishwa na kundi la wasanii tofauti wa Kiafrika.
Kwa mwaka huu Tamasha la Sauti za Busara
litafanyika kuanzia Februari 12 hadi 15, likiwa ni moja ya matamasha
saba bora duniani ambayo unatakiwa kushuhudia na idadi ya wageni katika
kipindi cha tamasha ikiendelea kuongezeka.
Mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmoud anasema
limekuwaurafiki na mataifa mengine duniani kwani mara zote limekua
likitoa kipaumbelekwa wote pia kwa wenyeji na mwaka huu wameshusha
gharama za viingilio kwa wenyeji kutoka Sh5,000 hadi Sh3,000.
“Kiingilio ni bure kwa wenyeji kabla ya saa 11
jioni na baada ya hapo ni Sh3,000 tu kwa Watanzania wote ili waweze
kuhudhuria tamasha. Zaidi ya hapo, watoto wanaruhusiwa kuingia bila
kutozwa chochote hivyo basi wenyeji wanachotakiwa ni kujitokeza na
kusherekea muziki wa Afrika na wakipeperusha bendera ya Tanzania, pamoja
na wageni,” anasema Mahmoud.
Anasema kwa kupitia mchango wa Sauti za Busara,
Tanzania inaendelea kujidhatiti katika ramani ya dunia katika suala zima
la utalii wa kiutamaduni.
“Sauti za Busara inawaleta watu pamoja, hutoa
ajira, inasaidia kuimarisha utamaduni wa asili, inaendeleza wasanii
pamoja na kukutana na kujifunza kutoka kwa wenzao, pia inatangaza utalii
wa kiutamaduni wa Tanzania. Mbali na hapo, Sauti za Busara inafanya
kazi kubwa katika nchi ikiwemo kukuza amani na umoja kwa kuheshimu
utofauti na mchanganyiko wa utamaduni mbalimbali,” anasema Mahmoud.
Licha ya kutajwa kwamba yanakuza utalii, matamasha
makubwa yanayofanyika hapa nchini yameelezwa kuwa na msaada katika
kuhamasisha vijana wadogo kupenda utamaduni wao. Mahmoud anasema hayo ni
baadhi ya mafanikio ya matamasha makubwa, ambayo pia hutoa fursa kwa
wanamuziki wa hapa nchini kuchangamana na kubadilishana mawazo na
wanamuziki kutoka mataifa mbalimbali.
Tamasha hilo ukiacha kutoa fursa za kutengeneza
mitandao kwa wasanii wa ndani, Serikali ya Tanzania imeonyesha katika
takwimu zilizotolewa tangu tamasha lianze mwaka 2004, utalii umekua kwa
kiwango kikubwa huku idadi ya watalii ikiongezeka hadi kufikia asilimia
500.
Shindano la kuimba laanzishwa
Tamasha la mwaka huu na likiwaleta pamoja wasanii tofauti na
watazamaji kusherekea muziki wa Kiafrika inahodhi shindano, kukiwa na
zawadi ya pesa taslimu ambayo ni pesa ya kurekodi kwa washindi wa nyimbo
za amani.
Mahmoud anasema, “Sauti za Busara 2015 litaisaidia
kukuza amani kwa kutumia muziki ambapo vikundi 15 kutoka Tanzania,
sambamba na vingine vya kimataifa vitatoa sauti za ujumbe wa amani,
umoja na mshikamano katika maonyesho yao. Tunatarajia kwamba (sauti)
hizi zitasikika kwa nguvu na uwazi.”
Anasema wasanii wa Kitanzania walioingia katika
shindano hilo ni pamoja na Leo Mkanyia, Msafiri Zawose, Mohamed Ilyas,
Zee Town Sojaz, Ifa Band, Mgodro Group, Mabantu Africa na wengine wengi.
“Shindano la Nyimbo za Amani litafanyika kati ya
saa 10:00 jioni Alhamisi ya Februari 12 na saa 2:00 usiku wa Jumapili ya
Februari 15. Shindano liko wazi kwa wakazi au wazawa wa Tanzania.
Vikundi vyote vya Kitanzania vinavyoshiriki kwenye tamasha vinaalikwa
kutunga nyimbo maalumu yenye dhima ya amani na umoja na kuifanyia
onyesho katika mida yao ya kutumbuiza katika tamasha,” anasema Mahmoud.
Anasema fedha taslimu zitazawadiwa kwa ajili ya
uzalishaji wa rekodi kitaalamu wa nyimbo zenye ubunifu: Sh4 milioni
(mshindi wa 1), Sh3 milioni (mshindi wa 2) na Sh2 milioni kwa mshindi wa
tatu.
Wakiwemo pamoja na wasanii wakubwa wa kimataifa
kama Blitz the Ambassador kutoka Ghana, tamasha litashereheshwa na
Tcheka (Cape Verde), Isabel Novella (Mozambique), Aline Frazao (Angola),
Octopizzo na wengineo.
Wasanii watakaowakilisha Tanzania katika Sauti za
Busara 2015 ni Ali Kiba, Msafiri Zawose, Leo Mkanyia, Culture Musical
Club, Mgodro Group, Mabantu Africa Ifa Band, Cocodo African Music na
wengineo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment