Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema
kuwa Kenya na Tanzania ni nchi zenye uhusiano wa muda mrefu hivyo kuna kila
sababu za kuendelea kuimarisha na kuitekeleza Sera ya Demokrasia ya Uchumi kwa manufaa ya pande mbili hizo.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo, huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na
Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya Mhe. John Michael
Haule, ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kuaga na kupata baraka za Rais.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Haule kuwa kwa vile Kenya na Tanzania zimo katika
mchakato wa kutekeleza Sera ya Demokrasia ya Uchumi ana matumani makubwa kuwa
mafanikio makubwa ya kiuchumi yataendela kupatikana baina nchi mbili hizo.
Dk. Shein alisema
kuwa mashirikiano katika nyanja mbali mbali za maendeleo hasa ikizingatiwa nchi
mbili hizo zimo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki yamekuwa yakiimarika siku
hadi siku.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa nchi mbili hizo zimekuwa na historia ya kusaidiana pale nchi moja
wapo inapopata matatizo, hivyo ana imani kubwa na Balozi Haule kuwa ataendeleza
uhusiano na ushirikiano huo kati ya nchi mbili hizo kutokana na utendaji wake
wa kazi.
Kwa upande wa
Zanzibar, Dk. Shein alimueleza Balozi Haule kuwa kumekuwa na uhusiano wa kidugu
na kihistoria kati ya nchi hiyo na Zanzibar hasa ikizingatiwa uhusiano kati ya
Zanzibar na Mombasa katika nyakati za ukoloni hatua ambayo imepelekea kuimarika
kwa uhusiano huo hadi hii leo na kuweza kuwepo kwa Ubalozi Mdogo huko mjini
Mombasa.
Dk. Shein alisema
kuwa hivi sasa Kenya na Zanzibar kumekuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri wa
kibiashara hasa katika zao la karafuu, ambapo wafanyabiashara wa nchi hiyo
wamekuwa wakinunua karafuu kupitia Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).
Alisema kuwa
hatua hiyo imeweza kuondosha tatizo lililokuwepo hapo siku za nyuma ambapo biashara
hiyo ilikuwa ikifanywa kimagendo na
baadhi ya watu kati ya Kenya na Zanzibar na kuikosesha Zanzibar kuimarisha pato
lake la uchumi.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi Haule haja ya kulitangaza soko
la Utalii nchini Kenya kwani nchi hiyo nayo imeweza kupata mafanikio katika
sekta hiyo.
Nae Balozi Mteule
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya Mhe. John Michael Haule
alimuahidi Dk. Shein kuwa katika utekelezaji wa Kazi zake nchini humo atazidi
kujenga uhusiano na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Kenya.
Balozi Haule
alieleza kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini humo utaimarisha zaidi uhusiano na
ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati katika kuhakikisha Sera ya
Demokrasia ya Uchumi kati ya pande mbili hizo inaimarishwa.
Katika mazungumzo
yake Balozi huyo, alisisitiza haja ya kuimarisha ulinzi katika maeneo ya Utalii
hapa nchini sambamba na kuimarishwa kwa usafiri kati ya Kenya na Tanzania ikiwemo
Zanzibar ili kutoa usafiri wa uhakika kwa wageni wanaotembelea vivutio vya
kitalii vilivyopo katika maeneo hayo.
Aidha, Balozi
huyo aliahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano katika nyanja ya uwekezaji na
biashara hasa ikizingatiwa kuwa katika nchi za Afrika ya Mashariki nchi ya
Kenya inaongoza kwa wawekezaji na wafanyabiashara wake kuekeza hapa Tanzania.
Pamoja na
hayo, mazungumzo hayo yalijikita katika
kuimarisha mambo mbali mbali ya kimaendeleo yakiwemo ya kiuchumi kati ya Kenya
na Tanzania.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment