Home » » ZEC LEO KUTAJA VYAMA VITAKAVYOSHIRIKI UCHAGUZI.

ZEC LEO KUTAJA VYAMA VITAKAVYOSHIRIKI UCHAGUZI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAKATI Chama cha Tanzania Democratic Alliance (TADEA) kikitangaza rasmi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Zanzibar, utakaofanyika Machi 20 mwaka huu, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) leo itaweka hadharani majina yote ya wagombea watakaoshiriki uchaguzi huo.

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utarudiwa baada ya ule wa Oktoba 25, mwaka jana kufutwa na ZEC kutokana na kasoro zilizogubika demokrasia hiyo muhimu. Katibu Mwenezi wa TADEA, Rashid Mshenga alithibitisha kushiriki kwa chama hicho baada ya kumaliza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri, akisema wamejiridhisha kwamba uchaguzi ndiyo mchakato pekee wa kidemokrasia wa kupata viongozi halali.
“Maamuzi ya mwisho tumekubaliana kushiriki katika uchaguzi wa marudio kwa sababu ndio mchakato na utaratibu pekee wa kidemokrasia wa kuwapata viongozi halali wa kuongoza nchi , baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana kufutwa,” alieleza Mshenga.

Alisema, chama hicho kitamsimamisha tena mgombea wake wa nafasi ya urais wa Zanzibar, Juma Ali Khatib na kitasimamisha wagombea katika baadhi ya majimbo kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

TADEA inaungana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Kijamii (CCK), Sauti ya Umma (SAU) pamoja na Tanzania Labour Party (TLP) kuweka wagombea katika uchaguzi wa marudio huku Chama cha Wananchi (CUF) kupitia mgombea wake wa nafasi ya urais, Maalim Seif Sharif Hamad kikisusia uchaguzi huo.

Kwa upande wake, ZEC kupitia Ofisa Mwandamizi ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema mchakato wa kupokea majina ya vyama vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo utakamilika leo ambao ndiyo siku ya mwisho.
“Tutaweka hadharani majina ya wagombea wote wa vyama vya siasa watakaoshiriki katika uchaguzi wa marudio leo baada ya kukamilika mchakato huo ambao unatoa nafasi kwa Tume ya Uchaguzi kuchapisha karatasi za kupiga kura,” alieleza ofisa huyo.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa