Home » » SERIKALI ZOTE MBILI ZA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR ZITAENDELEA KUJENGA MAZINGIRA MAZURI-BALOZI SEIF

SERIKALI ZOTE MBILI ZA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR ZITAENDELEA KUJENGA MAZINGIRA MAZURI-BALOZI SEIF

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina Ofisini kwake vuga Mjini Zanzibar.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina wa Pili kutoka Kushoto akimuelezea  Balozi Seif Mikakati ya Ofisi yake kuwajibika Zaidi Zanzibar katika dhana nzima wa kuimarisha Muungano wa Tanzania.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema kwamba Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kujenga mazingira mazuri ya uwezeshaji katika kuhakikisha lengo lililokusudiwa na Taifa la kupatikana kwa Katiba Mpya ya Tanzania linafanikiwa vyema.

Alisema jukumu la kuratibu kazi ya kupatikana kwa Katiba hiyo  kupitia kura ya Maoni itakayopigwa na Wananchi baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba itakuwa chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania          { NEC } na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC }. 

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina yaliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema Wananchi walio wengi Bara na Zanzibar bado wanaamini kwamba Tanzania inahitaji kuendelea kuongozwa na Serikali zinazozingatia haki ,usawa na Utawala bora na hili litapatikana zaidi iwapo Katiba Mpya itayokidhi vigezo hivyo itakamilika kwa mujibu wa Taratibu baada ya kupigiwa kura na Wananchi wenyewe.

Balozi Seif alieleza kwamba wakati Taifa linaelekea kujiandaa na mipango hiyo Serikali zote mbili zitakuwa tayari kupambana na kikundi au mtu ye yote atakayeonyesha dalili za kutaka kutishia amani ya Taifa iliyopo hivi sasa.

Alimueleza Naibu Waziri huyo wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Muungano na Mazingira na Ujumbe wake kwamba vyombo vya dola kwa pande zote mbili havitasita kuwashughulikia wale wote watakaoamua kutaka kuichezea amani ya Nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ukaribu wake wa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar uliopelekea kustawisha maendeleo ya Wananchi wa pande zote mbili.

Alifahamisha kwamba Watanzania wote ni wamoja. Hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kuimarisha Muungano uliopo wa pande hizo mbili ulioasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Aman Karume na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Aprili 26 Mwaka 1964.

“ Historia itaendelea kubakia ikionyesha kwamba Wananchi wa Tanzania na Bara na wale wa Zanzibar ni wamoja kutokana na muingiliano wa kidamu uliopo kabla ya hata ya kuja kwa Muungano uliopo sasa ”. Alisema Balozi Seif.

Akizungumzia Taasisi za Serikali ya Muungano zilizoamua kutaka kujenga majengo yake ya Kudumu Visiwani Zanzibar kwa lengo la Kuimarisha Muungano Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuzipatia maeneo ya ujenzi Taasisi hizo.
Alisema zipo Taasisi ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano pamoja na Kituo cha utafiti cha Taifa { COSTEC } tayari zimeshapatiwa maeneo na zimeshajenga Ofisi zao hapa Zanzibar.
Mapema Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kusimamia amani kabla na baada ya uchaguzi Mkuu.
Mh. Luhaga alisema rasilmali  nyingi  zilizopo nchini ambazo zinaendelea kufaidisha maisha ya Wananchi walio wengi bado zinasimama juu ya amani inayoendelea kusimamiwa na Serikali.
Katika kuimarisha Muungano Naibu Waziri Luhaga Mpina alimueleza Balozi Seif kwamba tayari ameshamuagiza Katibu Mkuu Wake kufanya utaratibu wa kumpatia Nyumba ya Kudumu Zanzibar  ili kumpa fursa ya kutekeleza majukumu yake kwa uhakika.
Alisema tabia ya kukodiwa hoteli kwa ajili ya makaazi yake anapokuwa Zanzibar kwa shughuli za kikazi  ikiwa ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni vyema itaachwa mara moja.
Mh. Luhaga alieleza kwamba yeye ni mshirika wa mazingira jambo ambalo anawajibika kufanya kazi akiwa karibu na Waziri mwenzake anayesimamia mazingira kwa upande wa Zanzibar.
Akikabidhi Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi  { NEC }kuhusu uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  mnamo Tarehe 23 Juni 2016  Ikulu Mjini Dar es salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Daniel Lubuva alisema Tume hizo zimepewa jukumu la kushughulikia kura ya Maoni.
Jaji Lubuva alisema kilichopo kwa sasa kwa watendaji wa Tume hizo ni kuangalia changamoto zilizomo ndani ya sheria ya kura ya Maoni nambari 11 ya mwaka 2013  kwa ajili ya kuandaa mswaada wa marekebisho utakaopelekwa Bungeni hapo baadae.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania aliwathibitishia Watanzania katika Mkutano huo kwamba kura ya Maoni itapigwa kama Katiba ilivyofafanua licha ya mabadiliko ya ratiba yake kuchelewa kutokana na kuingiliana na Uchaguzi Mkuu.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa