RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana aliungana
na Waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi mbali mbali katika Maulidi ya
kuadhimisha Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) kitaifa yaliofanyika katika viwanja
vya Maisara mjini Zanzibar.
Sherehe hizo za
kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanyika kila mwaka Kitaifa hapa
Zanzibar ni miongoni mwa kawaida na mila ya Waislamu wa Zanzibar.
Alhaj Dk. Shein
aliungana na Waislamu na wananchi hao wakiwemo viongozi mbali mbali wa Dini na
Serikali pamoja na wananchi ambapo pia, Mama Mwanamwema Shein nae alihudhuria Maulid
hayo akiwa pamoja na viongozi wengine wanawake wa Kitaifa.
Kadhi Mkuu wa Zanzibar
Sheikh Khamis Haji alitumia fursa hiyo kuwakaribishwa wananchi wote pamoja na
viongozi mbali mbali akiwemo Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein katika sherehe hizo za
Maulid.
Katika Sherehe hizo, Waislamu walisisitizwa suala zima la
amani, umoja na mshikamano miongoni mwao na kutakiwa kufuata nyayo za Mtume
Muhammad (S.A.W) ili wapate kuongoka hapa duniani na kesho akhera.
Akisoma khutba Sheikh Muhammed
Kassim Said kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana aliwataka Waislamu kuwa kitu kimoja huku akiwasisitiza
umuhimu wa kusaidiana na kuhurumiana kwa lengo la kupata rehema za
Allah.
Sheikh Muhammed pia,
alitumia fursa hiyo kukemea mambo maovu katika jamii hasa suala la unyanyasaji
wa wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na suala zima la ubakaji jambo ambalo
limeanza kushamiri hivi sasa katika jamii na kueleza athari zake na kutaka
mashirikiano ya pamoja katika kulipiga vita.
Aidha, alieleza kuwa
ni jukumu la Waislamu kusherehekea siku hii adhimu pamoja na kufuata mafunzo ya
Mtume Muhammad (S.A.W) aliyokuja nayo.
Sherehe hizo za Maulid
ambazo husherehekewa duniani kote, zilianza kufunguliwa na Qur-an tukufu
iliyosomwa na Ustadhi Iddi Ussi Haji
kutoka Tazari Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo tafsiri yake ilitolewa na
Ustadhi Ali Muobwa Hassan kutoka Chuo cha Kislamu Zanzibar.
Milango ya Maulid Barzanji iliyoenda sambamba na
Qasweeda ilisomwa na Maustadhi kutoka vyuo mbali mbali vya Qur-an kutoka Unguja
na Pemba yakiwemo Maulid ya Hom kutoka Jumuiya ya Maulid ya Hom Mtendeni, Mkoa
wa Mjini Magharibi ambayo nayo yalikuwa kivutio kikubwa katika sherehe adhimu.
Katika sherehe hizo za
Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) Ustadhi Abdul Rahman Habshi pamoja na
Madressa Al-Nur-Islamia ya Mkunazini, Mji Mkongwe walisoma Qiyam Talaa,
kilichotanguliwa na Mlango wa nne uliosomwa na Ustadhi Bakari Shukuru Makame
kutoka Jambiani Mkoa wa Ksuini Unguja,
Qasweeda ya mwaka 1438
Alhijra, ilisomwa na wanafunzi kutoka Madrassa Maamur ya Tumbatu Jongowe, Mkoa
wa Kaskazini Unguja ambapo Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya Maulid hayo Sheikh Sherali Chapsi alitumia fursa hiyo
kama ilivyokaida kwa kila mwaka kumkabidhi Rais, Qasweda hiyo maalum.
Maulid hayo
yalimalizika kwa Mlango wa dua uliosomwa na Sheikh Mwalimu Ali kutoka Tumbe,
Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na hatimae kufungwa kwa fatha iliyosomwa na
Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Mahmoud
Mussa Wadi chini ya mshereheshaji Sheikh Hamza Zubeir Rijal.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 comments:
Post a Comment