Imeandikwa na Khatib Suleiman, Zanzibar
MAMLAKA ya kupambana na kuzuia rushwa Zanzibar imeanza kutoa elimu
juu ya madhara ya rushwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
ambapo ndiyo watarajiwa wa viongozi wa baadaye.
Ofisa wa Elimu wa mamlaka hiyo, Shuwekha Abdalla Omar alisema tayari
jumla ya shule 30 zimefikiwa katika kazi ya kutoa elimu kuhusu rushwa na
majukumu ya mamlaka ya kupambana na rushwa.
Alisema kazi hiyo itaendelea hadi katika vyuo vikuu na taasisi za
elimu ya juu kwa wanafunzi wake kuweza kufahamu madhara ya rushwa kwa
jamii. “Kwa muda wa miaka miwili tumekuwa tukitoa elimu kwa makundi
mbalimbali kuhusu rushwa na madhara yake lakini pia watu waifahamu
mamlaka ya kuzuia na kupambana na rushwa,” alisema.
Alisema katika utafiti wa hatua ya kwanza umeonesha kwamba jamii
inachukia rushwa pamoja na kufahamu madhara yake, lakini tatizo kubwa
watu hawapo tayari kufichua uovu huo. Omar alisema katika awamu ya pili
wanakusudia kuzifikia shule nyingi zaidi ikiwemo za vijijini kuanzia
msingi hadi sekondari.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment