Imeandikwa na Mwandishi Wetu
MKOA wa Mjini Magharibi Unguja na baadhi ya vitongoji vyake upo
katika hatua za mwisho za kutekeleza mradi mkubwa wa mji salama na
uwekaji wa kamera za ulinzi za CCTV.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohamed Mahmod alisema
hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juzi. Alisema mradi wa
uwekaji wa kamera za ulinzi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Unguja
lengo lake kubwa kuimarisha ulinzi na usalama kwa ajili ya kudhibiti
uhalifu.
Alifahamisha kwamba matukio ya uhalifu katika nyakati tofauti ndiyo
yaliyosababisha serikali kuanzisha mradi kuweka kamera za ulinzi na
udhibiti wa uhalifu. “Mradi salama wa uwekaji wa kamera katika mji wa
Zanzibar unaendelea vizuri ambao lengo lake kubwa kudhibiti matukio ya
uhalifu yanayotishia usalama wa wananchi na wageni,” alisema.
Alisema hivi karibuni alikuwepo Marekani katika ziara ya kuangalia
maendeleo ya mradi huo ikiwemo vifaa vitakavyotumika ikiwa ni sehemu ya
kujiridhisha. Baadhi ya vifaa ambavyo vimo katika makubaliano ya mradi
huo ni vya ukaguzi katika maeneo ya uwanja wa ndege wa Zanzibar na
bandarini.
Alisema kuwekwa kwa vifaa hivyo katika maeneo muhimu ya Mji Mkongwe
wa Zanzibar kutasaidia kufanya kazi za ukaguzi wa njia ya kisasa zaidi
tofauti na sasa kwa kutumia njia ya kupapasa ambayo wakati mwingine
huibua malalamiko kwa jamii.
Mohamed alisema vifaa vya mradi salama wa udhibiti matukio ya uhalifu
vitawekwa katika maeneo ya Mji Mkongwe na barabara zake pamoja na
maeneo ya vivutio yanayotembelewa na watalii.
“Matukio ya majambazi kupora na wahalifu kuwashambulia watalii kwa
kuwamwagia tindikali yalitia ndoa na kuathiri sekta ya utalii. Sasa
hatutaki yatokee tena na ndiyo maana tumewekeza mradi huu mkubwa wa
kamera za ulinzi,”alisema.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment