Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Picha ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa
(MB) katika picha ya pamoja na washiriki mbalimbali wa Mkutano wa 47 wa
maandalizi ya mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa msimu wa mvua za vuli
(Oktoba-Disemba 2017) kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (Greater
Horn of Africa Climate Outlook Forum-GHACOF-47), Zanzibar Beach Resort, tarehe
21-22 Agosti 2017
-------------------------------------------------------
“Napenda kuwapongeza GHACOF kwa kuwezesha sayansi
ya hali ya hewa kutumika katika shughuli za maendeleo ya jamii, nikiangalia kwa
upande wa nchi yetu ya Tanzania kumekuwa na ongezeko la mahitaji na matumizi ya
huduma za hali ya hewa kwa kiasi kikubwa sambamba na wigo mpana wa uelewa wa
matumizi ya taarifa hizo, ambapo inasaidia sana wananchi kukabiliana na
mabadiliko ya hali ya hewa,” haya aliyasema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB) wakati akifungua rasmi Mkutano wa 47 wa maandalizi
ya utabiri na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki
na Pembe ya Afrika (Forty Seventh Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum
(GHACOF-47) kwa msimu wa mvua za vuli wa mwezi Oktoka hadi Desemba 2017.
Katika mahojiano yaliyofanyika na Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi alielezea dhumuni la
kukutana kwa wataalamu wa mkutano huo kuwa ni kujadili, kukubaliana kwa pamoja
na kutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua za vuli kuanzia mwezi wa
Oktoba hadi Desemba 2017 kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.
Aidha aliongezea kuwa baada ya taarifa hiyo kutolewa kila nchi shiriki ikiwemo
Tanzania itakaa na kuandaa taarifa yake ambapo
kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) taarifa rasmi itatolewa kwa
vyombo vya habari mwishoni mwa mwezi Agosti 2017.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Kituo cha Ufuatiliaji
wa Hali ya Hewa cha Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (ICPAC) Dkt. Guleid
Artan akizungumza katika ufunguzi huo alisema, ICPAC kwa kushirikiana na
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wanatekeleza programu ya utoaji
wa tahadhari na kwa wakati (Integrated Regional Early
Warning System (IREWS))
ukiwa na lengo la kuhakikisha nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika
wananufaika kwa kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zitolewazo zinafika kwa
jamii kwa wakati na zinatumika katika kupunguza madhara ya yatokanayo na hali
mbaya ya hewa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Zanzibar Mhe.
Mwinyi Ussi Abdallah Hassan akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa
wa Mjini Magharibi aliwataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa kwa
karibu kwa kutumia njia za kisasa zilizopo.
GHACOF ni Mkutano unaowakutanisha
wataalamu wa hali ya hewa kama watoa huduma pamoja na wataalamu kutoka katika sekta
mbalimbali kama watumiaji kutoka nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika
kwa lengo la kujadili, kuandaa na kutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu
husika katika ukanda huu.
IMETOLEWA
NA: MONICA MUTONI, AFISA HABARI,
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
0 comments:
Post a Comment