BILIONEA wa Tanzania asiye na maneno mengi, zaidi ya vitendo katika
uwekezaji, Said Salim Bakhressa anayemiliki mtandao wa biashara za kila
aina ndani na nje yaAfrika Mashariki, ameibuka na kitu kipya
kinachotarajiwa kuiongezea thamani Tanzania katika sekta ya utalii.
Kitu hicho kipya ni mji wa kisasa wa Fumba wenye hadhi ya kimataifa
katika ufukwe wa Fumba nje kidogo ya Mji wa kitalii wa Kisiwa cha
Unguja, Zanzibar unaotarajiwa kuwa na nyumba za kisasa 720 zenye thamani
ya mabilioni ya shilingi. Hatua ya kwanza ya mradi imetumia Dola za
Marekani milioni 20 (Sh bilioni 42). Nyumba hizo zitajengwa katika eneo
litakalozungukwa na mtandao wa barabara za lami za kilometa 20 na aina
nyingine ya miundombinu ya kisasa.
Aidha mji utakuwa na huduma muhimu za kijamii kuanzia shule,
hospitali, masoko, hoteli, maduka makubwa, sehemu za kupumzikia zenye
michezo ya kisasa sehemu za ufukweni na baharini. “Utakuwa mji wa kisasa
na wa kitalii kwelikweli, mji wa kuigwa na gumzo kwa Afrika Mashariki
na nchi nyingine za Afrika,” alisema Mkurugenziwa Mawasiliano na
Uhusiano wa Kampuni za Bakhressa, Hussein Sufian aliyezungumza na
HabariLEOToleo la Afrika Mashariki.
Alisema tayari awamu ya kwanza ya ujenzi unaohusisha nyumba 150 iko
katika hatua za mwisho ikitarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, na
kwamba lengo la mradi huo ni kuchochea na kufungua fursa zaidi za
kiuchumi kupitia uuzaji bidhaa za ndani, kukuza sekta ya utalii, kuvutia
vituo vya uwekezaji, makazi ya kisasa na kadhalika.
Aliongeza kuwa, pamoja na kutanua wigo wa uwekezaji na utalii
utakaoihakikishia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuwa na `mafuriko’ ya
wageni katika mji huo wa kisasa na vivutio vingine vya utalii, mradi huo
utatanua pia wigo wa ajira, mapato ya Serikali huku akisisitiza; “Kama
mapato yakiongezeka, uwezo wa Serikali wa kutoa huduma kwa jamii
utaongezeka.
“Tunaamini Serikali yoyote imara ni ile inayohudumia vyema watu wake,
nasi tunadhani kupitia mradi huu tutachangia kwa kiasi kikubwa kukuza
uchumi wa nchi. Kwa mgeni atakayeingia Zanzibar, ataweza kujiona yuko
katika sehemu ya hadhi ya juu kama zilivyo sehemu nyingine za kitalii
duniani.” FAHARI YA NCHI Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji
Zanzibar (ZIPPA), Salum Khamis Nassoro akizungumzia mradi huo aliouita
ni fahari ya Zanzibar, alisema ni moja ya miradi takribani saba katika
eneo hilo linalotarajiwa kuwa na shughuli za kibiashara za kimataifa.
“Nathubutu kusema ni fahari ya Zanzibar, Bakhressa amefungua njia…
kwa hatua hii, ni lazima itafika wakati watu kutoka nchi mbalimbali za
Afrika wataona fahari kuja kufuata mahitaji yao Zanzibar badala ya
kwenda Dubai, kwani kila wanachokifuata huko kitapatikana Zanzibar.
“Miundombinu itakuwa ya uhakika, mwekezaji atashirikiana na Serikali
kujenga barabara ya kilometa nane kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Amaan Karume hapa Zanzibar, kutakuwa na mfumo maalumu wa mawasiliano ya
kisasa, hapa hautaona nyaya za umeme, za simu, sijui madishi ya
setilaiti juu ya nyumba, kila kitu kitafukiwa ardhini…,” alisema
Nassoro.
PATO LA TAIFA Kukamilika kwa miradi hiyo kivutio kwa utalii, watalii
na wawekezaji wa ndani nje, si kwamba kutainufaisha Zanzibar pekee
ambayo pato lake la taifa linategemea utalii kwa asilimia 27, sekta
inayochangia fedha za kigeni kwa asilimia 83, bali hata Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania kwa ujumla.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Tanzania Bara inayotenganishwa na
bahari ya Hindi kwa umbali wa kilometa 73 tu, sawa na maili 26, ina
utajiri wa vivutio, vikiwemo Mlima Kimanjaro ambao ndyio mrefu zaidi
barani Afrika ukiwa na urefu wa meta 5,895 sawa na futi 19,340 kutoka
usawa wa bahari.
Aidha, kuna vivutio katika hifadhi za taifa, baadhi zikiwa Serengeti,
Tarangire, Manyara, Mkomazi, Arusha, Gombe, Mahale, Katavi, Rubondo,
Saanane, Mikumi, Ruaha, Saadani na kadhalika. Mamlaka ya hifadhi ya
Ngorongoro, moja ya maeneo ya urithi wa dunia ambayo pia ni moja kati ya
maajabu saba ya dunia, ni kivutio kingine katika ardhi ya Tanzania.
Eneo hili ni la kipekee, ni mahali ambako wanyama na binadamu
wanaishi bila kudhuriana. Ndipo lilipopatikana fuvu la kwanza la
binadamu wa kale aliyeishi ndani ya Ngorongoro kipindi cha miaka milioni
1.7 iliyopita na fuvu, eneo la Olduvai. Katika hifadhi hii yenye
wanyamapori wakubwa takribani 25,000, wamo vifaru, viboko, nyumbu,
pundamilia, nyati, simba, fisi, chui na kadhalika.
Kwa ujumla, pato la taifa la Tanzania linachangiwa kwa asilimia 17 na
sekta ya utalii, hivyo kuimarika kwa vivutio zaidi ya utalii, kunatoa
fursa zaidi ya ukuaji wa kiuchumi kwa nchi, na bila shaka mwelekeo wa
Bakhressa katika kuijenga Zanzibar itafungua milango zaidi ya maendeleo,
yakiwemo katika sekta ya utalii.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment