Na.Ali Issa na Zalha Kassim – Maelezo Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inatafuta mwekezaji mwengine katika eneo la Mangapwani wilaya ya kasikazini “B” Unguja baada ya Shirika la Agakhan Foundation kushindwa kuliendeleza eneo hilo ambalo walikodishwa na Serikali kwa lengo la kuliendeleza.
Hayo yamesemwa leo huko Baraza La Wakilishi Zanzibar na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi Haji Makame wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma (CCM) aliyetaka kujua hatma ya mwekezaji huyo ambaye kashindwa kuliendeleza eneo hilo kwa muda mrefu.
Dk.Mwinyi Haji akijibu swali hilo amesema kwamba mkataba wa mradi huo umefutwa tokea mwaka 2008 baada ya kusimamishwa mkataba wa kukodishwa ardhi kutokana na muekezaji huyo kushindwa kutekeleza yale aliyoagiza.
Aidha alisema kuwa kutokana na mradi huo kufutwa kabisa na muwekezaji kushindwa kuomba kurejeshewa kwa mradi huo serikali inatafuta mwekezaji mwengine ambae ataweza kuliendeleza eneo hilo kwa kuweka miradi mbalimbali .
Dk.Mwinyi Haji alisema kwamba, kwa sasa Serikali imepokea maombi mengi kwa waekezaji wengine kwaajili ya kuliendeleza eneo hilo ili kutimiza azma ya kuwawezesha wananchi wa Mangapwani kupata ajira.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Thuwaiba Edington Kisasi amesema kuna viashiria vinavyoonesha kuongezeka kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi Pemba kutokana na ujazo wa fedha uliojitokeza kwa sababu ya mavuno ya Karafuu.
Thuwaiba aliyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayuob aliyetaka kujua iwapo bei mpya ya Karafuu imesaidia kuinua kipato cha wakulima.
Thuwaiba amevitaja viashiria hivyo vya kiuchumi kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa ujenzi wa nyumba za kudumu na za kisasa,kuongezeka kwa ununuzi wa vipando kama vile magari na pikipiki na ongezeko la uanzishwaji wa miradi midogo midogo ya maendeleo.
Kikao hicho kidogo cha Baraza la Wawakilishi kimenza jana katika Ofisi zake zilizoko Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo inatarajiwa kuchukua muda wa wiki mbili.
0 comments:
Post a Comment