Home » » Watu 30 wapandishwa kizimbani kwa kosa la kusababisha vurugu Zanzibar

Watu 30 wapandishwa kizimbani kwa kosa la kusababisha vurugu Zanzibar

Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar

Watu 30 wakiwemo wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe  wakikabiliwa na makosa mbalimbali ikiwemo kuwashambulia Polisi,kuchoma moto matairi ya Magali barabarani na ukorofi.

Mbali na tuhuma hizo,pia wameshtakiwa kwa kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali kinyume na sheria pamoja na uzembe na ukorofi wa kuwashambuliya polisi kwa mawe.


Watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama nne tofauti, ikiwemo mahakama ya hakimu Mohammed Ali Mohammed walikofikishwa watuhumiwa wawili, wanne kwa hakimu Janet Nora Sekihola, 11 kwa hakimu Omar Mcha Hamza na 11 waliobakia, wamepandishwa mbele ya hakimu Valentine Andrew Katema.

Kwa nyakati tofauti watuhumiwa hao walishitakiwa kwa makosa ya kufanya mikusanyiko isivyo halali, uzembe na ukorofi pamoja kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani.

Watuhumiwa hao ni Mbarouk Said Khalfani (45), na Mussa Juma Issa (57) wanaodaiwa kuwa ni viongozi wa Jumuiya hiyo, ambapo walifikishwa mbele ya hakimu Mohammed Ali Mohammed, na kusomewa shitaka la kufanya mkusanyiko isivyo halali kinyume na kifungu cha 55 (1) (2) (3) na kifungu cha 56 cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Wengine ni Mbwana Hamadi Juma (50), Massoud Hamadi Mohammed (17), Mohammed Juma Salum (35), Abdulrahman Simai Khatib (19), Hashim Juma Issa (54) Matar Fadhil Issa (54).

Watuhumiwa hao kwa upande wao wamefikishwa katika kizimba cha mahakama ya hakimu Mdhamini Janet Nora Sekihola kujibu shitaka uzembe na ukorofi kinyume na kifungu cha 181 (d) cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Wengine walifikishwa katika mahakama ya hakimu Omar Mcha Hamza na Valentine Andrew Katema, wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani.

Wakiwa mahakamani hapo, watuhumiwa hao walishitakiwa chini ya kifungu cha 74 (1) (b) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Mashitaka yote hayo yaliwasilishwa kwa nyakati tofauti na Waendesha Mashitaka, Wanasheria wa serikali Mohammed Kassim Haasan, Suleiman Haji Hassan pamoja na Ramadhan Abdallah, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Katika mahakama ya hakimu Mohammed Ali Mohammed, Mwendesha Mashitaka Mohammed Kassim alidai kuwa watuhumiwa Mbarouk Said na Mussa Juma, bila ya halali walipatikana wakiandamana kupitia katika maeneo mbali mbali ya Manispaa ya mji wa Zanzibar.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Mei 26 mwaka huu majira ya saa 6:30 za mchana huko Lumumba wilaya ya Mjini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, shitaka ambalo hata hivyo walilikana mahakamani hapo.

Kwa upande wa watuhumiwa sita waliofikishwa katika mahakama ya hakimu Janet Sekihola, Mwendesha Mashitaka Suleiman Haji alidai kuwa watuhumiwa hao walifanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka huyo, kitendo hicho ni cha kuchoma moto mipira ya gari barabarani pamoja na kuwarushia mawe askari Polisi, baada ya kukusanyika isivyo halali katika barabara ya Michenzani wilaya ya Mjini Unguja, majira ya saa 1:00 za usiku wa Mei 26 mwaka huu.

Katika mahakama zote hizo, watuhumiwa hao walisimamiwa na Wakili wa Kujitegemea Abdallah Juma, ambapo aliiomba mahakama hizo kuwapatia wateja wake dhamana, kwa mujibu wa kifungu cha 150 (1) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar.

Watuhumiwa waliofikishwa mbele ya hakimu Omar Mcha Hamza na Valentine Andrew Katema, Mwendesha Mashitaka Ramadhan Abdallah kwa nyakati tofauti aliwasomea watuhumiwa hao mashitaka ya kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani.

Wote hao kwa pamoja walidaiwa kupanga mawe barabarani, kuchoma moto mipira ya gari barabarani pamoja na kuwarushia mawe askari, kitendo ambacho kingeweza kuleta uvunjifu wa amani.

Matukio hayo yametokea Mei 27 mwaka huu, majira ya saa 7:00 za mchana katika maeneo ya Mfereji wa wima na Amani wilaya ya Mjini Unguja.

Upelelezi wa mashauri yote hao bado haujakamilika kwa mujibu wa Waendesha Mashitaka wa mahakama hizo, na kuomba yaahirishwe ili waweze kukamilisha upelelezi wake.

Mahakama zote hizo zilikubaliana na hoja hizo za upande wa mashitaka, na kuziahirisha kesi hizo hadi Juni 11 mwaka huu kwa kutajwa.
Hadi redio hii inaondoka mahakamani hapo, kulikuwa hakuna hata mmoja aliyetoka kizuizini, licha ya mahakama hizo kuwapatia masharti ya dhamana.

Masharti hayo ni bondi ya shilingi 300,000 na wadhamini watatu waliotakiwa kusaini bondi ya kiwango kama hicho cha fedha kwa kila mdhamini, ambapo mmoja kati yao awe ni mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Masharti hayo yametolewa kwa watuhumiwa wawili waliofikishwa mbele ya hakimu Mohammed Ali Mohammed, ambapo sambamba na masharti hayo wadhamini hao pamoja na watuhumiwa wenyewe wametakiwa kuwasilisha kopi ya hati ya kusafiria, barua za Sheha wa Shehia wanazoishi pamoja na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Hakimu Janet Sekihola, Omar Mcha Hamza na Valentine Andrew Katema, kila mmoja aliwataka watuhumiwa hao kujidhamini kwa bondi ya shilingi 500,000 na wadhamini wawili wenye vitambulisho watakao wasilisha kiwango kama hicho cha fedha taslimu, na hakimu Valentine kuongeza kuwa mmoja kati ya wadhamini hao awe ni mfanyakazi wa SMZ.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa