Home » » Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar akutana na Ujumbe wa umoja wa Makanisa Tanzania

Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar akutana na Ujumbe wa umoja wa Makanisa Tanzania



Na Miza Chande-Maelezo Zanzibar



Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed ameuhakikishia umoja wa Mapadri nchini kuwa malamiko ambayo wameyatoa kwa Serikali atayawasilisha kwa maandiko kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohammed Shein.

Malalamiko hayo yanatokana na vurugu ambazo zilitokea mwishoni mwa wiki katika maeneo ya mji wa Zanzibar ambapo Makanisa matatu yalichomwa moto na kusababisha uharibifu wa mali mbali mbali za Makanisa.

Waziri Aboud ameyasema hayo alipokutana na Ujumbe wa umoja wa Makanisa Tanzania ulioongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Dk. Valontine Mokiwa katika Afisi ya Waziri huyo Mjini Zanzibar.

Amesema Serikali na kila mwananchi mpenda amani amehuzunishwa sana na fujo zilizotokea na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kufanya kazi yake ya kuwatafuta wale wote waliohusika na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Waziri Aboud amesema amefurahishwa na subra ambayo Wakristo hao wameichukua bila ya kulipiza kisasi jambo ambalo linawajengea heshima kubwa kwa jamii. 

Amezisisitiza Taasisi za dini kuendelea kuhubiri amani kama lengo la taasisi hizo linavyosema na kuongeza kuwa kama kuna mambo ambayo yanafaa kuzungumzwa ni suala la ukosefu wa ajira na umasikini nchini.

Amesema Viongozi wa Dini wanapaswa kuwa na mipaka,busara na elimu wa yale wanayoyahubiri na kuwataka wananchi kuweza kuchambua juu ya viongozi ambao wanafaa kusikilizwa na wale ambao hawafai kusikilizwa.

Aidha amewahakikishia Viongozi hao wa dini kuwa na amani na kwamba ulinzi umeimarishwa katika Sehemu zao za ibada ili kuweza kuzuia watu ambao hawaitakii mema Zanzibar.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Dk. Valontine Mokiwa amesema kuwa matukio ambayo yamekuwa yakifanyika yamepindukia mpaka Zanzibar lakini Serikali ya Mapinduzi imekuwa imeonekana kuwa na imani kubwa wakati hali inakuwa mbaya.

Amdai kuwa Makanisa 25 katika Visiwa vya Unguja na Pemba tokea mwaka 2001 yameshambuliwa lakini hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa kwa wahalifu hao jambo ambalo linawapa shaka.

Mokiwa amesema Jamii ya Wakristo nchini ina hamu ya kujua nani kahusika na kuchukuliwa hatua za kisheria na siyo tu kuishia kuambiwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta wahalifu hao.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa