Home » » WATORO BARAZA LA WAWAKILISHI KUNYIMWA POSHO YA VIKAO

WATORO BARAZA LA WAWAKILISHI KUNYIMWA POSHO YA VIKAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeshauriwa kuwanyima posho ya vikao vya baraza Wajumbe wa  Baraza hilo wenye tabia ya utoro.
Ushauri huo umetolewa na  Makamo  wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Balozi Seif Ali Iddi,  kutokana na kuchukizwa na tabia za wajumbe wa baraza hilo kutohudhuria vikao.

Wakati akifunga kikao cha Baraza la Wawakilishi jana, Balozi Seif  aliutaka uongozi wa Baraza hilo kutazama upya mfumo wa utoaji wa posho za vikao vya baraza  ili  kuwabana Wawakilishi wenye tabia  ya utoro.

“Ni aibu kuona wajumbe nusu ya  baraza hili hawamo bila ya sababu za msingi ni vyema tabia hii ikomeshwe,” alisema Balozi Seif.

Balozi Seif alisema si vyema kwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kukwepa majukumu yake ya msingi kwa kukimbia vikao vya baraza hilo isipokua kwa sababu za msingi zinazokubalika kwa mujibu wa kanuni za Baraza hilo.

Alisema kitendo cha Spika au Mjumbe yeyote anayeongoza kikao hicho kuahirisha vikao vya baraza mara kwa mara kutokana na  sababu ya mahudhurio yasiyoridhisha ni jambo lisilokubalika kidemokrasia, kiuchumi, na kisiasa.

Alisema tabia hiyo ya utoro kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  inakidhalilisha chombo hicho kikubwa mbele ya macho, masikio na midomo  ya wananchi wanaowawakilisha majimboni mwao na taifa kwa ujumla.

Alisema kitendo hicho cha utoro kinawanyima haki wananchi kusikia na kuona mambo yao yanazungumzwa na kutafutiwa ufumbuzi unaofaa.

“Kwa mujibu wa  Kanuni ya 74(2) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi, mjumbe yeyote ambaye bila ya dharura inayokubalika na Spika au Mwenyekiti wa Kamati  atashindwa kushiriki katika Kikao cha Baraza na Kamati zake  hatolipwa posho kwa ajili ya kikao hicho na endapo posho kwa  ajili ya kikao hicho imelipwa mapema , atakatwa kutoka kwenye stahili zake nyingine zitakazolipwa baadae”alisema Balozi Seif.

Juzi Spika wa baraza la wawakilishi Pandu Ameri Kificho alilazimika kuahirisha kikao cha baraza hilo kutokana mahudhurio yasioridhisha ya wajumbe wa baraza hilo.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kimeahirishwa hadi  Oktoba 22, mwaka huu  baada ya kupitisha bajeti  ya serikali  inayokadiria kutumia bilioni 707.8.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa