Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MTOTO
Milembe Matius mwenye umri wa miaka sita, mkazi wa Mwera Mabonde ya
Mpunga visiwani Zanzibar ameshambuliwa kwa kupigwa pamoja na
kuchanjwachanjwa vidole vyake viwili vya mkono wa kulia na mama yake
wakambo.
Mtoto huyo ambaye
anasoma darasa la tatu katika Shule ya Maandalizi alipatwa na mkasa huo
juzi huko nyumbani kwao Mwera Mabonde ya Mpunga majira ya asubuhi.
Akizungumza na
waandishi wa habari huko katika Hospitali ya Mnazi mmoja alipokuwa
akipatiwa matibabu mtoto huyo alisema kuwa, mama yake huyo alimpiga
pasipo kosa lolote.
Alisema kuwa, pamoja na
kumpiga kwa siku hiyo pia mama huyo alikuwa na kawaida ya kumpiga kila
siku na kumtishia asimwambie baba yake mzazi kwa madai kuwa atampiga.
"Kila siku amekuwa
ananipiga na juzi alinichinja kwa kisu wakati namenya chungwa, lakini
aliniambia nisimwambie baba na nikisema atanipiga," alisema.
Hata hivyo, kwa upande
wake baba wa mtoto huyo, Shija alisema kuwa ameanza kuona afya ya mtoto
wake ikibadilika, lakini kila anapojaribu kumwambia mke wake huyo huwa
haelezi ukweli wowote.
Alisema kuwa, kikawaida
yeye huondoka wakati wa asubuhi na kwenda katika shughuli zake za kila
siku na kurejea jioni, lakini juzi wakati anarudi alikuta nyumbani
hakuna mtu na alipojaribu kufuatilia aliambiwa na majirani kuwa mtoto
wake amepigwa na kuhifadhiwa kwa majirani.
Alisema kuwa, wakati
alipofika huko alimkuta mwanaye akiwa ameumia sehemu za usoni na kupata
michubuko na alipomuuliza alimwambia amepigwa na mama yake.
Alifafanua kuwa, wakati
anamkuta mwanawe yupo katika hali hiyo mke wake huyo hakuwepo na
alirejea nyumbani majira ya saa 2:00 usiku na alipomuuliza ni sababu
gani ya kumpiga mtoto kiasi hicho alijibu kuwa yeye hajampiga.
"Mara baada ya kumkuta
mtoto wangu katika hali hiyo, hatua niliyochukua ni kupiga ripoti polisi
(kupeleka taarifa polisi) na asubuhi tukaenda kituoni na hivi sasa mke
wangu huyo yupo kituo cha Polisi," alisema.
Akizungumza kwa masikitiko baba wa mtoto huyo Shija alisema kuwa, kitendo hicho kimemuathiri sana na hakiwezi kuvumilika.
Naye Daktari ambaye
anahusika na fomu namba tatu ya polisi (PF3), Salim Omar Mbaruok alisema
kuwa amemfanyia uchunguzi mtoto huyo na kusema kuwa, amepata majeraha
katika paji la uso na vidole vyake viwili vya mkono wa kulia vimechanjwa
na kitu chenye ncha kali.
"Ni majeraha ya kawaida
yaliyo sababishwa na kitu chenye ncha kali na hiyo michubuko pamoja na
kuumia katika paji lake la uso," alisema.
Hata hivyo alisema
kuwa, matatizo ya udhalilishaji yapo kwa kiasi kikubwa na ni ya kutisha
hali ambayo wanahitaji watu kupatiwa elimu zaidi ili kuachana nayo.
Alisema kuwa, kitengo
chake kimekuwa kikishughulikia masuala yote ya udhalilishaji ambapo kwa
siku hupata kesi karibu ya 10, huku Wilaya ya Magharibi ikiongoza kwa
matukio hayo.
Naye Ofisa Dawati la
Jinsia na Watoto, Sajenti Haji Mohammed Iddi alisema kuwa, juzi alipokea
taarifa ya mtoto kupigwa na mama yake wa kufikia na alipojaribu
kufuatilia wamefanikiwa kumtia hatiani na hivi sasa wamo katika kufungua
jalada ili ikiwezekana mtuhumiwa afikishwe mahakamani.
Hata hivyo, mtoto huyo
hali yake inaendelea vizuri na mara baada ya kupatiwa matibabu
aliruhusiwa na mama huyo akiwa yupo katika kituo cha polisi mjini hapa
0 comments:
Post a Comment