SAKATA
la uchotaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo wiki iliyopita
Bunge limeridhia wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo wawajibishwe,
bado limeendelea kutikisa nchi.
Bunge hilo liliridhia mapendekezo manane yaliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Bw. Zitto Kabwe.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuitaka mamlaka ya uteuzi iwawajibishe Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliachim Maswi.
Maalim Seif-Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Zanzibar imepata athari kubwa kwa kukosa fedha za wafadhili kutokana na wizi wa fedha katika akaunti hiyo ukihusisha baadhi ya viongozi wa Serikali ya CCM.
Maalim Seif aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mkokotoni, Jimbo la Tumbatu, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema miongoni mwa miradi iliyoathirika kutokana na nchi wahisani (wafadhili), kusitisha misaada baada ya kuibuka kwa kadhfa hiyo ni mradi wa Millennium Challenge Corporation, unaosaidia huduma za umeme na ujenzi wa barabara.
Aliongeza kuwa, Zanzibar ilikuwa ikinufaika na misaada ya kibajeti na ile inayotolewa na Mfuko wa Dunia na hakuna Mzanzibari aliyetajwa kunufaika na fedha hizo; hivyo kama wangekuwa na mamlaka kamili, athari hizo zisingewakuta kama ilivyo sasa.
Nape na msimamo wa CCM
Katika hatua nyingine, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Bw. Nape Nnauye, amesema chama hicho kinaheshimu maamuzi ya wabunge kutaka watu wote waliohusishwa na sakala hilo wawajibishwe.
Aliitaka Serikali iwachukulie hatua kwani CCM ni chama kinachofuata maadili ya uongozi hivyo hawawezi kuwa wa kwanza kutetea watu wanaofanya maovu serikalini.
“Kashfa mbalimbali zimewahi kutokea zikihusisha baadhi ya viongozi serikalini ambao waliwajibika,” alisema. Bw. Nnauye aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa Mnarani, Manispaa ya Mtwara na kusisitiza kuwa, CCM itaendelea kulinda maadili yake kama chama.
Escrow yaibua mazito Songea
Katika hali isiyo ya kawaida, baadhi ya wananchi mjini Songea, mkoani Ruvuma, wamegoma kuchangia fedha za ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule za sekondari.
Hali hiyo inatokana na kuibuliwa kwa wizi wa fedha katika Akaunti ya Escrow wakidai fedha zilizochotwa zingetosha kujenga vyumba vya maabara kwa sekondari zote nchini.
Mkoa huo una upungufu wa maabara 361 ambapo wananchi wanatakiwa kuchangia sh. 2,000 hadi sh. 10,000 kila mmoja.
Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti wilayani humo jana, baadhi ya wananchi walidai hawapo tayari kuchangia fedha za ujenzi wa maabara wakidai Serikali imeshindwa kuwabana viongozi wanaotuhumiwa na wizi huo hadi sakata hilo limekuja kuibuliwa bungeni.
“Kwa mujibu wa Katiba ya nchi, wananchi wana haki ya kudai au kugomea kitu chochote kama watabaini kinakwenda kinyume bila kuathiri taratibu na sheria.
“Sisi wakazi wa Songea tulihamasika kuitikia agizo la Rais Jakaya Kikwete kuhusu ujenzi wa vyumba vya maabara katika sekondari zetu lakini sakata la Escrow limetufanya tukate tamaa ya kuchangia,” alisema mwananchi mmoja.
Bw. Imani Mapunda (28), mkazi wa Mjimwema-Lizaboni, alisema wananchi wana haki ya kugoma kuendelea kuchangia ujenzi huo kama Serikali itashindwa kutekeleza maazimio manane yaliyoamuliwa na wabunge.
Maazimio hayo ni pamoja na kuwafukuza kazi baadhi ya Mawaziri waliotajwa kwenye ripoti ya PAC na kusisitiza wabunge waliohusika kuwatetea wahalifu, nao waachie ngazi kabla wananchi hawajatoa hukumu.
“Tunamkumbuka hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye katika kipindi chake cha utawala, alikuwa hana mchezo na viongozi wanaohujumu mali za umma bali aliwakamata na kuwafungulia mashtaka,” alisema Mapunda.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Joseph Mkirikiti, hakuweza kupatikana ofisini kwake ili kusikia maoni yake baada ya wananchi kugoma kuchangia ujenzi wa maabara ikidaiwa alikuwa nje ya ofisi kwa shughuli za kikazi.
BAWACHA walia na Pinda
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) Tanzania Bara, Bi. Hawa Mwaifunga, amesema CCM imemlinda Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ili asiwajibishwe na kutenguliwa uteuzi wake.
Alisema kama Bw. Pinda angewajibishwa katika sakata la uchotaji fedha kwenye akaunti hiyo, chama hicho kingeingia aibu na kusababisha Baraza la Mawaziri kuvunjwa.
Bi. Mwaifunga aliyasema hayo Zanzibar juzi wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Magogoni, Wilaya ya Magharibi Unguja na kuongeza kuwa, wabunge wa CCM wamekuwa wakisimama kidete kutetea uchafu unaofanywa na viongozi wanaotokana na chama chao.
“Wa t anz ani a wanapaswa kutambua kuwa, baadhi ya wabunge wa CCM, hawapo bungeni kutetea masilahi ya wananchi badala yake wanatetea uovu kwa masilahi yao.
“Katika sakala la Escrow, wamemlinda Pinda wakihofia aibu ya kuvunjwa Baraza la Mawaziri mara mbili...awali lilivunjwa baada ya kuibuka sakala la Kampuni ya Richmond ambapo aliyekuwa Waziri Mkuu kipindi kile, Bw. Edward Lowassa alijiuzulu, baraza likavunjwa,” alisema.
Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, Bi. Mwaifunga alisema BAWACHA imepanga kuzunguka nchi nzima ili kutoa ujumbe kwa CCM kuwa Rasimu ya Katiba waliyoipitisha haijazingatia matakwa ya Watanzania.
Alisema Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, amekuwa mstari wa mbele kuwashawishi Wazanzibari waipigie kura ya ndio akidai Katiba hiyo ni nzuri jambo ambalo si kweli.
“Namshangaa Dkt. Shein anapoipigia debe Katiba ambayo haijatokana na matakwa wa Wazanzibari na Watanzania bila shaka hajaisoma...naomba aisome kwa makini ili aweze kuwaambia Wazanzibari ukweli,” alisema.
Aliongeza kuwa, Watanzania lazima waikatae Katiba hiyo ambayo imezingatia maoni ya CCM badala ya wananchi.
Naye Katibu Mkuu wa BAWACHA, Bi. Grace Tendega, aliwataka Wazanzibari kuacha itikadi zao za vyama badala yake waungane pamoja kuitetea nchi yao.
Alisema Zanzibar ni nchi inayohitaji kuwa na mamlaka yake ambayo yataweza kupatikana kama wanawake wataungana, kuwa mstari wa mbele kwa kuikataa Katiba Pendekezwa.
Mwigulu Nchemba atema cheche Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Taifa, amesema wote waliohusika kuchota fedha kwenye akaunti hiyo lazima wachukuliwe hatua za kisheria.
Alisema fedha hizo zimetokana na kodi ya wananchi hivyo viongozi wenye dhamana serikalini ambao wametajwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC), watawajibishwa na wengine kufukuzwa kazi. Bw. Nchemba aliyasema hayo juzi wakati akiwasimika na kuwaapisha Makanda na Manaibu wake wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) mkoani Mara.
Miongoni mwa Makamanda waliosimikwa ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, Bw. Christopher Kangoye na Naibu wake, Bw. John Ginta, ambaye pia na mchumi wa chama hicho katika Wilaya ya Tarime, mkoani humo.
Hafla ya kuwasimika na kuwaapisha, ilifanyika kwenye Viwanja vya Musoma mjini ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na CCM.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment