Home » » MAALIM SEIF AFICHUA SIRI CCM

MAALIM SEIF AFICHUA SIRI CCM

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kina mkakati maalumu wa kudumaza maendeleo ya wananchi waishio katika mikoa ya Kusini na kusababisha iwe na hali mbaya kiuchumi zaidi ya miaka 52.

Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyasema hayo juzi wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Tunduru kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Baraza la Iddi, mkoani Ruvuma.

Maalim Seif alisema mikoa hiyo imebahatika kuwa na rasilimali za kutosha hususan bahari inayoweza kutoa ajira kwa vijana hasa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, mazao ya korosho na ufuta ambayo ni ya kibiashara.

"Pamoja na wakazi wa mikoa hii kulima korosho kwa wingi hakuna soko la uhakika, hivi sasa linaonekana kama halina faida... suala la gesi nalo limegeuka kuwa janga badala ya neema ili kupunguza ukali wa maisha," alisema.

Maalim Seif alisema Wilaya ya Tunduru haina miundombinu mbali ya kuwa na rasilimali za kutosha kama madini ya aina mbalimbali lakini wakazi wake wanaishi maisha magumu.

"Nimesafiri kwa gari kutoka Masasi mkoani Mtwara hadi hapa tukiwa mwendo kasi lakini tumetumia saa nne kwa umbali wa Kilomita 252...CCM haina sera nzuri kwenye kilimo ndio maana wakulima hawatazamwi na hawana thamani," alisema Maalim Seif.

Aliongeza kuwa, hakuna mkakati wa kuwahudumia wakulima ambapo katika suala la matumizi ya rasilimali na maliasili ya nchi, hakuna sera ya kuwanuifaisha Watanzania badala yake zinawanufaisha wageni kuliko wenyeji.

Alisema kama CUF kitapata ridhaa ya wananchi ili kuongoza Serikali, kitabadilisha sera ya uwekezaji, kuanzisha sera ambayo itakuwa na manufaa kwa Watanzania moja kwa moja.

"Tutaanzisha utaratibu wa makusanyo ya mapato yatokanayo na rasilimali na maliasili za nchi kama madini mbalimbali, dhahabu, gesi na kupanga matumizi katika makundi manne.

"Robo ya mapato hayo, itaingia kwenye mgawo wa wananchi moja kwa moja na robo tatu iliyobaki itaingia kwenye matumizi ya kujenga nchi," alisema.

Maalim Seif alisema, CUF wanaamini kama kila Mtanzania atapata mgawo ambao utatokana na mapato ya maliasili za nchi, atakuwa mlinzi wa kwanza kulinda rasilimali hizo na uwajibikaji wa viongozi na Serikali utaongezeka hivyo aliwaomba wananchi wakiunge mkono chama hicho.

Katika hatua nyingine, wakazi wa Kata ya Mchopeka wilayani humo, wameilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwapelekea huduma za afya kwenye kata hiyo badala yake Kituo cha Afya kilichojengwa Kijiji cha Njenga, kimegeuzwa ghala la kuhifadhia korosho.

Wakisoma taarifa yao kwa Maalim Seif, walisema inasikitisha kuona Serikali imeshindwa kuboresha huduma za afya katika kata hiyo na kuwaacha wananchi wakiendelea kupoteza maisha kwa kukosa huduma muhimu za tiba.

Akizungumzia hali hiyo, Bw. Rashidi Rajabu alisema jengo hilo ambalo limejengwa miaka mitano iliyopita, limeshindwa kufunguliwa badala yake linatumika kama ghala hivyo walimuomba Maalim Seif afuatilie jambo hilo ili waweze kupata huduma za afya.

Naye Bi. Mariamu Mkukusi kutoka Kata ya Mchopeka, alisema kuna kituo kingine cha afya katika kata hiyo ambacho hakina dawa wala watumishi wa kutosha hivyo kusababisha watu kupoteza maisha hasa wanawake wajawazito na watoto.

Akihutubia mkutano wa hadhara, Maalim Seif aliwataka wakazi wa kata hizo kutambua kuwa, sera mbovu za Serikali ya CCM ndizo zimewafikisha Watanzania katika umaskini walionao.

Alisema mbali ya Wilaya hiyo kuwa na ardhi nzuri pamoja na rasilimali za kutosha, watu wake ni maskini na kupata huduma za jamii kwa shida hivyo aliwataka wawe tayari kubadilika na kutoirudisha CCM madarakani.

Aliwataka wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Makazi ili walete mageuzi ya ushindi kuanzia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2015 kwa nafasi za udiwani, ubunge na urais.

"Chagueni viongozi wa Serikali za Mitaa ambao watatoka kwenye vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)... msiwape kura CCM," alisema.

Aliongeza kuwa, vyama vya upinzani vimedhamiria kwa thati kupambana na CCM ambapo utafiti walioufanya umeonesha ushirikiano huo utaleta mabadiliko pamoja na kupata ushindi katika mitaa mingi kutokana na CCM siku zote kushinda kwa kura chache na upinzani wakigawana kura

Chanzo;Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa