MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zaharani Hamad amewataka wafamasia kwenda katika Bohari Kuu kuchukua dawa zinazotumiwa na akinamama wajawazito kupambana na maradhi mbalimbali ambayo husababisha vifo.
Hamad alisema hayo wakati alipozungumza na wafamasia na wafanyakazi wa vituo vya afya vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na hospitali za binafsi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuyafikia Malengo ya Milenia ya kupunguza vifo kwa akinamama, imeweka kipaumbele cha kwanza cha kupambana na vifo vinavyotokana na akinamama kwa kuwapatia dawa za kujilinda na maradhi hatari.
“Matumizi ya dawa za akinamama na watoto kujilinda na maradhi mbalimbali hatari ndiyo yanayotakiwa kutumiwa na madaktari katika kipindi cha ujauzito,” alisema.
Daktari Mkuu wa mradi wa kupambana na vifo vinavyotokana na akinamama wajawazito, Ali Omar alisema kama wafamasia na madaktari watatumia dawa za akinamama wajawazito kujilinda na maradhi hatari, vifo vinavyotokana na maradhi hayo itakuwa ndoto.
Kwa mfano alisema madaktari katika vituo vyote wanatakiwa kutumia dawa za kuwalinda watoto kutoka akinamama na ugonjwa hatari wa Ukimwi ambazo zipo.
“Malengo ya serikali pamoja na Milenia ni kuondosha moja kwa moja maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda watoto ifikapo mwakani ambapo mafanikio yake yatapatikana tu kama akinamama watatumia dawa hizo,” alisema.
Aidha alisema mafanikio hayo yatafikiwa tu kama akinamama watafika katika vituo vya afya kuchunguza afya zao mapema kabla ya kujifungua na wakigundulika kuwa na matatizo hayo kutumia dawa sahihi.
Baadhi ya wafamasia kutoka katika vituo vya afya vinavyomilikiwa na vikosi vya ulinzi wameitaka Bohari Kuu kuwapatia huduma hizo ambazo zimekosekana kwa muda mrefu.
Amina Haji kutoka katika Hospitali ya Kikosi cha KMKM alisema hospitali yao inatoa huduma kwa asilimia kubwa kwa wananchi wanaoishi jirani na vituo hivyo na sehemu nyingine ambapo dawa za akinamama kujilinda na maradhi hayo zinahitajika.
“Tunaiomba Bohari Kuu ya Serikali kuzitupia jicho hospitali zinazomilikiwa na vikosi vya ulinzi ambazo zinatoa huduma kwa asilimia kubwa kwa wananchi binafsi,” alisema.
Lengo la mafunzo ya wiki moja kwa wafamasia kutoka sekta binafsi na Serikali ni kujenga mtandao utakaosaidia kufanya kazi kwa ushirikiano na kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Chanzo:Habari Leo
0 comments:
Post a Comment