WANAHARAKATI na jumuiya mbalimbali wameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzifanyia marekebisho haraka sheria zinazokandamiza uhuru wa wanawake na watoto kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mwandamizi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar Asha Abdi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku 16 za kupiga vita ukatili wa kijinsia kwa wanawake.
Alisema zipo sheria ambazo zimekuwa kikwazo kwa wanawake zikichangia kuongezeka kwa kasi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na hivyo kurudisha nyuma juhudi za wanawake kupata maendeleo.
Kwa mfano aliitaja Sheria ya Mahakama ya Kadhi nambari 3 ya mwaka 1985 ambayo ipo katika mchakato wa marekebisho imekuwa ikikwamisha wanawake kupata haki katika ndoa zaidi wakati mwanamke anapoachika katika ndoa.
“Zipo sheria zinaongoza kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia nchini ikiwemo Sheria ya Mahakama ya Kadhi ambayo inawanyima wanawake haki za mgao wa mali wakati wanapopewa talaka,” alisema.
Salama Sadatti wa Jumuiya ya Walemavu Wasioona alisema Sheria ya Ushahidi inatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa kwani hadi sasa haitambuwi ushahidi wa mtu mwenye ulemavu wa akili wakati wa kutoa ushahidi Mahakamani.
Akifafanua zaidi alisema upo ulemavu wa aina nyingi ambapo wapo walemavu wenye matatizo ya akili wenye ufahamu mkubwa wa kutambua mambo mbalimbali na uwezo wa kuzungumza.
“Tumewasilisha malalamiko yetu muda mrefu kutaka Sheria ya Ushahidi ya mwaka 1917 ifanyiwe marekebisho na kuutambua ushahidi wa mtoto mwenye matatizo ya ulemavu Mahakamani,” alisema.
Alisema udhaifu wa sheria hizo kwa kiasi kikubwa umetoa mwanya kwa wahalifu ikiwemo wabakaji kuelekeza nguvu zao kuwabaka watoto wenye matatizo ya ulemavu.
Tamwa kupitia Mradi wa Kuwawezesha Wanawake na Jinsia (GEWEP) kwa kushirikiana naShirika la Kimataifa la Care Tanzania na Zanzibar Gender wanakusudia kufanya matukio mbalimbali ikiwemo makongamano kwa kuwashirikisha watu mbalimbali kuelimisha na kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment