OFISI ya Msajili wa Ardhi inakusudia kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba kwa watu ambao hadi sasa wameshindwa kukamilisha zoezi la usajili wa nyumba zao pamoja na rasilimali.
Msajili wa Ardhi Mwanamkaa Abrahman alisema wamechukua uamuzi huo kwa lengo la kuona wanamaliza zoezi hilo ambalo limepata baadhi ya vikwazo vilivyopelekea kudorora.
Alivitaja vikwazo vilivyopelekea kushindwa kukamilisha zoezi la usajili wa ardhi ni pamoja na baadhi ya nyumba kukodishwa, migogoro ya ardhi katika familia na baadhi ya nyumba kukosa hati miliki ya waraka.
“Zoezi la usajili wa ardhi katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mji Mkongwe limekabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwemo wamiliki wenyewe kukodisha nyumba zao na migogoro ya kifamilia,” alisema.
Alisema katika kukamilisha zoezi hilo wanakusudia kuanzisha vituo vidogo katika eneo la Mji Mkongwe vitakavyofuatia kwa karibu sana kukamilisha zoezi hilo.
Alivitaja vituo vitakavyofanya kazi na kukamilisha zoezi hilo kwa haraka kuwa ni Mlandage, Mji Mkongwe, Miembeni na Malindi.
“Tumeamua kuanzisha vituo vidogo vidogo ambavyo vitasaidia kukamilisha zoezi la usajili wa ardhi kwa haraka sana huku tukiyapatia ufumbuzi malalamiko yanayotokana na migogoro ya kifamilia,” alisema.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha utaratibu mpya wa kusajili ardhi kwa ajili ya matumizi sahihi ya wananchi kwa lengo la kupunguza migogoro iliyotawala katika familia.
Migogoro ya ardhi imetawala zaidi katika maeneo ya uwekezaji ya fukwe za utalii mwambao wa pwani kutokana na ardhi kuongezeka thamani kwa matumizi mbalimbali.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment