SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetakiwa kutowafumbia macho
watendaji wa taasisi wanaokwamisha au kuchelewesha miradi ya wawekezaji
kiasi ya kuwavunja moyo.
Hayo yalisemwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wakitoa
maoni kuhusu mradi mkubwa wa uwekezaji katika sekta ya utalii huko
Matemwe unaotekelezwa na Kampuni ya Penny Royal.
Mwakilishi wa Jimbo la Welezo, Hassan Khamis Hafidh alisema ni aibu
kuona serikali imefungua milango kwa wawekezaji kuwekeza, lakini bado
vipo vikwazo mbalimbali ambavyo ni chanzo cha kuwavunja moyo wawekezaji
sawa na kuwepo dalili za rushwa.
Mratibu wa mradi huo, Saleh Mohammed Said alisema wanapambana na
vikwazo mbalimbali katika utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo mlolongo wa
kodi na madai mbalimbali kutoka kwa wananchi ambayo hayana msingi na
uhalali.
Alisema wameshindwa kupata vibali vya kazi kwa wafanyakazi wa kigeni,
kitendo ambacho kimerudisha nyuma maendeleo ya ujenzi wa mradi huo
kuanza kikamilifu.
“Hatujaridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kijiji cha
utalii cha Matemwe kwa sababu ya urasimu mkubwa, ikiwamo milolongo ya
kodi.....hadi sasa hatujapata kibali cha wafanyakazi wetu wa kigeni
kufanya kazi Zanzibar,” alisema.
Aidha, alisema wamekuwa wakidai fidia mbali mbali kutoka kwa
wanakijiji wa eneo hilo ambapo inaonesha wazi wazi kwamba wananchi
hawajafahamu umuhimu wa mradi huo kwa maisha na maslahi ya wakazi wa
kijiji hicho ikiwemo kuzalisha ajira.
Mkurugenzi Mkuu wa Mradi huo, Brian Thompson alisema, wanakusudia
kujenga kijiji cha utalii cha mfano ambacho kitakuwa na huduma zote
ikiwamo ya uwanja wa ndege utakaorahisisha watalii kufika hapo moja kwa
moja. Aidha, alisema mradi huo unakusudia kutoa ajira kwa wananchi wa
Zanzibar huku ukilenga wanakijiji cha Matemwe wapatao 1,500.
“Mradi huu umelenga kuongeza pato kwa Serikali katika Sekta ya utalii pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wa Zanzibar,” alisema.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid alisema, sekta ya
utalii ndiyo tegemeo la taifa katika kuingiza fedha za kigeni na
kuzalisha ajira kwa vijana kwa hivyo serikali na taasisi zake zinatakiwa
kujenga mazingira mazuri yatakayowavutia wawekezaji kuwekeza.
0 comments:
Post a Comment