RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amevitaka Vyuo Vikuu hapa nchini kuwa makini katika usajili
wa wanafunzi wanaojiunga vyuoni humo kwa kuhakikisha wanakidhi viwango
vinavyohitajika katika ngazi za Taifa na Kimataifa.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika Chuo Kikuu cha Zanzibar University, kilichopo Tunguu,
Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja katika hotuba yake aliyoitoa katika
Mahafali ya 14 ya chuo hicho.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisema kuwa hivi karibuni kumeibuka baadhi ya vyuo vinavyosajili
wanafunzi bila ya kufuata viwango husika jambo ambalo linaharibu sifa ya elimu
na maendeleo ya wananchi na nchi kwa jumla hali ambayo itapelekea kupata wataalamu
wasiokuwa na sifa hapo baadae.
Alisema kuwa kuwepo
kwa ushindani mkubwa wa kutafuta wanafunzi wapya wanaotaka kujiunga katika vyuo
vya ndani na nje ya nchi isiwe sababu ya kuharibu ubora wa elimu kwa kusajili
wanafunzi wasio na viwango kuingia katika Vyuo Vikuu.
Aidha, Dk. Shein
alivitaka Vyuo Vikuu hapa nchini kuhakikisha kuwa kila mafunzo wanayotoa
yanakuwa na Wahadhiri na vifaa vya kutosha sambamba na kuwa na uwezo wa
kuendesha mafunzo hayo ili kuepuka kutoa elimu isiyokidhi haja.
Alisema kuwa mambo
hayo kwa pamoja ni muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa hapa
Tanzania.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa ubora wa elimu inayotolewa ni suala la mashirikiano kati ya jamii, vyuo na
serikali na kuhimiza haja kwa Vyuo Vikuu vya Zanzibar kufanya kazi karibu zaidi
katika kuhakikisha elimu inakidhi mahitaji yaliokusudiwa na wanafunzi nao
wanakidhi viwango.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kuwataka wazee kuendelea na malezi bora ya watoto wao sambamba na
kuwa karibu na maendeleo yao ya elimu huku akiwahakikishia kuwa Serikali
itaendelea kutoa elimu bure pamoja na kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa ya
kujiunga na elimu ya juu.
Aidha, aliwahakikishia
kuwa Serikali inafanya mageuzi katika mfuno wa elimu ili uende sambamba na
mahitaji ya nchi pamoja na mabadiliko ya Teknolojia yanayotokea duniani kote.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alisikitishwa na hali ya udanganyifu iliyofanywa na baadhi ya wanafunzi kwa
Bodi za Mikopo hapa nchini ambao walifika hatua ya kutoa taarifa zisizo na ukweli
hali ambayo huwanyima fursa wanafunzi wenye sifa na dhamira ya kweli ya kutaka
kuendelea na masomo pamoja na kusababisha hasara kwa Serikali.
Kutokana na hali hiyo,
Dk. Shein alisema kuwa ilimlazimu kuchukuwa hatau za dharura kusitisha utoaji
wa mikopo kwa muda lakini hata hivyo, alisema kuwa baada ya kuridhishwa na
kufikia hatua zinazohitajika aliruhusu Bodi ya Mikopo ya Zanzibar iendelee
kutoa mikopo kwa mwaka 2016/2017 huku akiitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali kuielimisha jamii juu ya suala zima la mikopo na hatari za udanganyifu.
Hivyo Dk. Shein
aliwataka wanafunzi wafahamu kwamba kufanya udanganyifu katika suala la mikopo
ni kosa la jinai hivyo aliwataka kujiepusha na
mambo hayo na kuwasihi kuitumia vyema mikopo wanayopewa kwa malengo
yaliokusudiwa.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alifurahishwa na taarifa ya kuwepo kwa mashirikiano mazuri kati ya vyuo
vya Zanzibar kikiwemoChuo Kikuu cha Zanzibar University, Chuo Kikuu cha Taifa
cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha SUMAIT, hatua ambayo inajumuisha
mashirikiano katika ufanyaji tafiti na ubadilishanaji wakufunzi.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisema kuwa hivi karibuni alitia
saini hadharani Mswada wa Sheria ya utafiti na uchimbaji wa Mafuta na Gesi
Zanzibar, hatua ambayo itaiwezesha Zanzibar kuanza taratibu za kuchimba mafuta
na gesi yake wenyewe na kuvitaka vyuo vikuu hapa nchini kuitumia fursa hiyo
katika kuunga mkono juhudi hizo za maendeleo kwa kuanzisha programu zitakazo
husiana na mafuta na gesi.
Vile vile, Dk Shein
alivitaka vyuo vikuu hapa nchini kutilia mkazo elimu ambayo itamuwezesha
muhitimu kuweza kujiajiri na kujitegemea mwenyewe badala ya kusubiri ajira
kutoka serikalini.
Dk. Shein alitoa
pongezi na shukurani kwa uongozi wa chuo hicho kwa kukiimarisha chuo chao kwa
kiasi ambacho kimepelekea ongezeko kubwa la wahitimu mwaka huu wapatao 1440 idadi ambayo ni zaidi ya mara mbili ikilinganishwa
na ile ya mwaka jana iliyokuwa 667 huku
akipongeza kwa kuazishwa programu mpya katika ngazi ya Uzamili na Uzamifu.
Pia, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuwasihi wahitimu hao kwa kuwataka wawe makini katika hatua
nyengine ya maisha wanayoingia hivi sasa ambapo baadhi ya wakati watalazimika kutafakari
na kuchukua maamuzi juu ya masuala muhimu na magumu katika maisha yao bila ya
kupata miongozo ya wazazi na walimu wao.
Aliwataka mkuazia sasa
wafahamu kwamba elimu waliyonayo ndiyo sialaha muhimu wanayoihitaji kuitumia
katika kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha na kufanya maamuzi
yanayozingatia busara na hekima ili waweze kufuzu katika maisha yao.
Aidha, aliwataka wahitimu
hao kutochagua kazi hasa wakizingatia kuwa soko la ajira limekuwa na ushindani
mkubwa na kuwataka kufikiri namna
ambavyo wataweza kuitumia na kunufaika na mifuko mbali mbali iliyoanzishwa na
Serikali kwa lengo la kuwasaidia vijana na makundi mbali mbali ili waweze
kujiajiri wenyewe na kukuza maendeleo ya ujasiriamali hapa nchini.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma
alitoa pongezi kwa uongozi wa chuo hicho kutokana na kuendeleza utamaduni mzuri
wa kutoa ufadhili kwa wanafuzi wa Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu hatua ambayo
imesaidia kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini.
Waziri huyo pia,
alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa kurejesha mikopo kwa wanafunzi
wanaokopa kupitia Bodi ya Mikopo ya Zanzibar ili fedha hizo ziweze kuwasaidia
wanafunzi wengine.
Makamo Mkuu wa Chuo
hicho Profesa Mustafa Rashash nae alitumia fursa hiyo kueleza mashirikiano
yaliopoa kati ya chuo hicho na Serikali pamoja na vyuo vyengine na kueleza
wanavyothamini juhudi za serikali katika kuendeleza sekta ya elimu hapa nchini.
Hata hivyo, Profesa
Rashash alieleza namna ya chuo hicho kilivyojipanga katika kuimarisha programu
zake mbali mbali chuoni hapo zikiwemo mpya na zile za zamani kwa lengo la
kukuza sekta ya elimu sambamba na kuendelea kukipa hadhi zaidi chuo hicho.
Profesa Saleh Idris ambaye
ni Kaimu wa Bodi ya Chuo hicho kwa upande wake alieleza azma ya chuo hicho
kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya afya kwa kuanzisha Digrii ya Uuguzi ambapo wahitimu 53 ni
miongoni mwa waliohitimu mahafali ya mwaka huu.
Pamoja na hayo,
Profrsa Idris kwa niaba ya chuo walitumia nafasi hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa
kuchaguliwa kwa kipindi cha Pili kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza
la Mapinduzi huku akieleza mikakati ya chuo hicho katika kuongeza majengo
yakiwemo ya daghalia.
Viongozi mbali mbali
walihudhuria katika Mahafali hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balaozi Seif
Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mkuu wa Chuo hicho
Profesa Suleiman Bin Nasry Basahal, Wakuu wa Vyuo mbali mbali,Mawaziri na
viongozi wengine kadhaa.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 comments:
Post a Comment