Home » » Wakulima wazawadiwa na Dkt Shein Pemba

Wakulima wazawadiwa na Dkt Shein Pemba


Na:- Azizi Simai Maelezo 
Pemba

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amewapongeza wakulima wa  zao la karafuu Zanzibar kwa kuweza kuliuzia Shirika la Taifa la Biashara  Zanzibar (ZSTC)karafuu kuliko ilivyotarajiwa kwa msimu huu.
  
Mheshimiwa Rais aliyasema hayo wakati alipokuwa akitowa zawadi ya Vyeti kwa Wakulima ,Mikoa, Wilaya na Shehia zilizofanya vizuri katika Uchumaji na uuzaji wa karafuu.
  
Katika Mkutano huo uliofanyika  nje ya Viwanja vya Ukumbi wa Jamhuri Wete Pemba  hivi leo Dkt Shein alimkabidhi Cheti Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Major Mstaafu Juma Kassim Tindwa  kwa kuwa Mkoa Bora wa Uchumaji na Uuzaji wa Karafuu ambapo  Kiwilaya Wilaya ya Wete ilikuwa Wilaya Bora wakati Shehia Bora ni Shehia ya Finya kutoka Wilay ya Micheweni.

Aidha Dkt Shein aliwakabidhi vyeti Wakulima wanne wa Karafuu ambao waliliuzia Shirika la ZSTC karafuu nyingi  msimu huu ambao ni Hamad Said Hamad, Said Ali Juma, Husein Khamis Jabu na Mohd  Issa Salim. 

Akiwapongeza Wakulima hao na Wananchi wa Zanzibar kwa ujumla amesema kuwa Serikali katika msimu huu ilipanga kununuwa Tani za karafuu 3000 zenye thamani ya Shs Billioni 33 badala yake imenunuwa tani 4758 zenye thamani ya shs Billioni 71. 

Kutokana na hali hiyo yakuvuka lengo iliojiwekea Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweza kupata  faida na pia wananchi kufaidika na bei  nzuri iluiotolewa na Serikali ya Shs 15,000/- kwa kilo moja ya karafuu ambayo inaendelea hadi sasa. 

Dkt Shein alirejea wito wake kwa Kuwataka wananchi kuiunga mkono Serikali yao kwa kuimarisha mashamba yao nakupanda Mikarafuu mipya huku Serikali nayo kwa upande wake itajitahidi kuhakikisha kuwa changamoto zote zilizojitokeza katika msimu huu itakabiliana  kwa kuyapatia ufumbuzi hatuwa kwa haruwa.  

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI PEMBA
17/4/2012. 

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa