Home » » Dk. Shein apokelewa na mabango

Dk. Shein apokelewa na mabango



Sakata la migogoro ya ardhi Zanzibar limechukua sura mpya, baada ya Rais Ali Mohamed Shein, kupokewa kwa mabango ya kupinga kitendo cha serikali kumpa mwekezaji ardhi maeneo ya Mchangamle, Kizimkazi.
Dk. Shein ambaye alimaliza ziara ya siku tatu katika mkoa wa Kusini Unguja jana, alilakiwa kwa mabango ya kumtaka aingilie kati mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji wa Hoteli ya Residence na wananchi wa Kizimkazi Dimbani, mkoa wa Kusini Unguja.
Baadhi ya mabango hayo yalibeba ujumbe wenye maandishi, ‘Mheshimiwa Rais tunaomba kurudishiwa eneo tulilonyaganywa barabarani’.

Jingingine lilisomeka, ‘ Mheshimiwa Rais tumechoka kunyanyaswa na kamati ya maendeleo ya Kizimkazi  ndani ya ardhi yetu ya Zanzibar’.
Pia mabango hayo yalitaka kufanyike haraka uchaguzi wa uongozi katika serikali ya kijiji cha Kizimkazi kutokana na uongozi kushindwa kushughulikia kero za wananchi wake.
Wakizungumza na NIPASHE moja kati ya watu waliokuwa wamebeba mabango hayo walisema kwamba, wamelazimika kutumia njia hiyo kufikisha ujumbe kwa Rais kutokana na viongozi wa wilaya na mkoa kushindwa kutatua mgogoro huo.
Akifanya majumuisho ya ziara yake katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Tunguu, Dk. Shein, aliwataka viongozi walioanzisha migogoro ya ardhi katika maeneo yao kuhakikisha wanaimaliza haraka.
Alisema analazimika kuwapa nafasi viongozi hao kumaliza mgogoro huo kabla ya mwenyewe kuamua kuingilia kati.
Wakati huohuo.  Dk. Shein, ametangaza kufuta ada za uzazi  kwa mama wajawazito  ili kufanikisha mpango wa serikali wa kupunguza vifo kwa mama wajawazito na watoto Zanzibar.
Dk. Shein alitangaza hatua hiyo jana, alipokuwa akizungumza na watendaji wa serikali katika mkoa wa Kusini Unguja, baada ya kumaliza ziara yake ya siku tatu ya  kukagua mafanikio na matatizo katika mkoa huo.
Alisema kuanzia sasa ni marufuku kwa kina mama wajawazito kutozwa ada hiyo na gharama zote zitabebwa na serikali ili kuwaondolea kero wananchi hasa wanyonge.

Rais Dk Shein alisema kwamba Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  zimeweka mpango wa kupunguza vifo kwa mama wajawazito na watoto na hatua ya kufuta ada ya Sh.  40,000 itasadia kufanikisha mpango huo.

“Huduma za uzazi zifanyike bure katika hospitali zote Zanzibar”alisisitiza D.k Shein.

Aidha, alisema utaratibu wa kuwataka mama wajawazito kuchangia huduma za upasuaji hauna tija yoyote katika kufanikisha mpango wa kupunguza vifo vya mama wajawaziti na watoto Zanzibar.
Dk. Shein alisema kwamba, mapato yanayopatikana  kupitia ada za upasuaji kwa mwaka karibu Sh. milioni 20 ni kiwango kidogo na serikali haiwezi kushindwa kufidia pengo hilo.
“Kina mama wajawazito watafanyiwa upasuaji bure kuanzia sasa na mahitaji yote yatabebwa na serikali yao.”aliongeza kusema Dk. Shein.
Alisema kwamba mashirika makubwa ya kumataifa ikiwemo Unicef yamekuwa yakisadia kufanikisha mpango wa kupunguza vifo kwa mama wajawazitio na watoto na hatua hiyo itasadia kuharakisha utekelezaji wa mpango huo katika muda mfupi.
Aidha Dk shein alisema kwamba katika mwaka wa fedha 2012/13 Serikali imeamua kuongeza bajeti ya dawa na mahitaji mengine ikiwa ni utekelezaji wa mpango wake wa kuimarisha huduma ya afya kwa wananchi wake.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa