Home » » ZANZIBAR KUPUNGUZA TATIZO LA AJIRA

ZANZIBAR KUPUNGUZA TATIZO LA AJIRA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk  .Ali Mohamed Shein,akizungumza na  wanayakazi wa Sekta mbali mbali za Serikali na Sekta Binafsi wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEY DAY)zilizofanyika jana katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja,(kushoto) Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar,Zahrani Mohamed Nassor,(kulia) Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na Waziri wa Kazi,Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Haroun Ali Suleiman, {Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.}.

Na Ramadhani Ali /Habari Maelezo 
          1.5.2012           Mayday

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inaendeleza  juhudi zake katika kupambana na changamoto kubwa ya tatizo la ajira nchini ambalo limekuwa likizikabili nchi nyingi duniani hasa nchi zinazendelea na inalichukulia tatizo hilo kuwa ni ajenda yake kuu hivi sasa katika mipango yake ya maendeleo.

Hayo yameelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohd Shein alipokuwa akizungumza na wafanyakazi katika kilele cha sherehe za wafanyakazi  duniani (Mei mosi) kwenye ukumbi wa Salama Bwawani.

Amesema  serikali ilijiwekea lengo la kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira, lakini bado kiwango cha ukosefu wa ajira hasa kwa vijana ni kubwa na limefikia asilimia 17 kwa mujibu wa taariifa ya utafiti wa Kaya uliofanywa mwaka 2009/2010.

Amesema pamoja na upungufu wa ajira uliopo bado, vijana wa Zanzibar wanafursa na uwezo wa kutumia nafasi za utandawazi na soko la ukanda wa Afrika Mashariki kuweza kupata ajira nje ya nchi.

Aidha Dk. Shein amewataka vijana wasisubiri ajira za serikali peke yake na wawe tayari kujiajiri wenyewe katika sekta mbali mbali ambazo serikali imeziimarisha ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji.

Rais wa Zanzibar amekemea tatizo la ajira za watoto ambalo baadhi ya watu wanalichukulia kama ni mbinu mojawapo ya watoto kusaidia familia zao kupambana na ugumu wa maisha bila ya kuangalia athari zinazoweza kutokea za kuwanyima haki yao ya elimu na nikwenda kinyume na sheria za kimataifa zinazolinda uhai na haki za watoto.

Amesema utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kwamba tatizo la ajira za watoto limefikia asilimia tisa ya idadi ya watoto wa Zanzibar na idadi kubwa hushirikishwa katika shughuli za kilimo, biashara ndogo ndogo, mifugo na uvuvi.

Kuhusu tatizo la mfumuko wa bei hasa za vyakula amesema serikali imekuwa ikikabiliana nalo kwa kuimarisha kilimo hasa cha umwagiliaji maji  na kupunguza bei ya pembejeo na huduma za matrekta ili kuongeza  uzalishaji wa chakula na kupelekea unafuu wa bei ya bidhaa nyengine.

Ameongeza kuwa Serikali imeanzisha utaratibu wa kuzungumza na wafanyabiashara wa bidhaa za chakula ili kushirikiana nao katika kupanga bei ambazo zinazingatia hali za wananchi ingawa baadhi yao wamekuwa hawafuati mpango huo na wengine huzisafirisha bidhaa zao kwa njia ya magendo ambazo wamelipia ushuru mdogo hapa Zanzibar.

Dk. Shein amesema serikali ya awamu ya saba imepiga hatua kubwa katika kuimarisha amani na utulivu nchini hivyo amewataka wafanyakazi na wananchi kwa jumla kujiepusha na vitendo vinavyoashiria kuvuruga amani iliyopo  na amewashauri kutumia fursa za majadiliano ya pamoja ili kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayojitokeza.

Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na wafanyakazi kutoka mawizara, maidara na mashirika ya serikali na binafsi Rais Ali Mohd Shein amesema kwa kutambua umuhimu wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbali mbali kujenga mazingira mazuri ili waweze kuzalisha zaidi na ameahidi kuongeza kima cha chini cha mshahara kila hali itakapo ruhusu na amesisitiza uwajibikaji na kuongeza uzalishaji.

Katika risala ya wafanyakazi iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la wafanyakazi  Zanzibar Maalim Khamis Mwinyi Mohd wamelalamikia pengo kubwa la mishahara lililopo baina ya wafanyakazi wa kawaida na wafanyakazi wa ngazi za juu pamoja na kutoshirikishwa katika utaratibu wa kupanga mishahara mipya iliyotolewa na serikali hivi karibuni.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya sherehe za wafanyakazi (mei mosi) mwaka huu ni mfumko wa bei, kodi kubwa na mishahara duni ni pigo kwa wafanyakazi.      
                              

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa