Home » » SIKUJIUZULU KWA SHINIKIZO - HAMAD

SIKUJIUZULU KWA SHINIKIZO - HAMAD


na Mauwa Mohammed, Zanzibar
ALIYEKUWA Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad, amesema hakujiuzulu kwa shinikizo la mtu yeyote bali ni kujenga heshima yake, chama chake na ya serikali anayoitumikia.
Hamad alibainisha hayo jana katika mkutano unaondelea katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Alisema anapingana na sababu iliyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Hamza Hasan Juma, aliyesema kujiuzulu kwake kumetokana na kutosimamia vema majukumu yake.
“Wala sikujiuzulu baada ya kamati ya ulinzi na usalama kukaa; niliandika barua kabla ya kamati hiyo kukaa. Mimi ni kiongozi wa kisiasa nalinda heshma yangu, ya chama changu na serikali ninayoitumikia,” alisema Hamad.
Alibainisha siku ya tukio alikuwa ofisini na kwamba baada ya kupata taarifa alichukua juhudi za kutafuta boti na kwenda eneo la tukio; na kuanza kazi ya uokoaji kama mmoja watu waliokuwa katika msafara huo.
Alisema kitendo cha kuambiwa wamechelewa si cha msingi, kwani ajali haitoi taarifa.
Alisema kabla hajachukua uamuzi ya kujiuzulu, aliwajulisha viongozi wake, Maalim Seif Sharif, Profesa Ibrahim Lipumba na Machano Khamis na kumtaka awape muda na baadaye walimkubalia.
Sambamba na hilo, alimpongeza Rashid Sefu, Mwakilishi wa CUF Jimbo la Ziwani kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kuahidi kushirikiana naye.
Watu mbalimbali wamepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na kiongozi huyo kuwa ni ya kijasiri na kishupavu ambayo ni mfano wa kuigwa na viongozi wengine.
Hamad alijiuzulu baada ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit inayamilikiwa na kampuni ya Seagull Julai 18 mwaka huu karibu na kisiwa cha Chumbe na kuua watu zaidi ya 100.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa