Home » » Tume ya ajali ya boti Z’bar yatajwa

Tume ya ajali ya boti Z’bar yatajwa



Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ametangaza tume ya kuchunguza ajali ya boti ya MV Skaigit  iliyopinduka na kuzama baharini kisha kuua watu 83 na wengine 61 hawajulikani walipo tangu kutokea ajali hiyo Julai 18, mwaka huu.



Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu,  Dk Abdulhamid Yahya Mzee, Rais Shein ameunda tume hiyo kwa kuzingatia sura 33 ya sheria ya Tume ya Uchunguzi ya Zanzibar.

Dk. Mzee alisema tume hiyo itafanyakzi ya kuchunguza chanzo cha boti hiyo kuzama, watu kupoteza maisha na wengine kuokolewa katika mwambao wa Bahari ya Hindi wa Pungume Zanzibar.

“Rais wa Zanzibar ameunda tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa boti ya Skagit kwa mujibu wa sherua ya Tume ya uchunguzi ya Zanzibar,”alisema Mzee.

Aliserma tume hiyo itakuwa na wajumbe 10  wakiwemo wataalamu wa masuala ya uokozi baharini na meli wakiongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Abdulhakim Ameir Issa.

Jaji Abdulhakim na wezake waliongoza tume ya uchunguzi ya ajali ya Meli ya MV Spice Islanders ambayo iliyozama katika mkondo wa bahari ya Nungwi na kuua watu 1,529 na watu 941 waliokolewa na wengine 1,000 waliripotiwa kupotea katika ajali hiyo Septemgba 10, mwaka jana.

Aliwataka wajumbe wa tume hiyo ni Meja Jenerali Said Shaaban Omar, Komando Hassan, Mussa Mzee,   Kepteni Abdallah Yussuf,  Kapteni Abdulla Juma Abdulla, Salum Toufiq Ali  na Kepteni hatib Katandula.

Wengine ni Mkakili Fauster Ngowi Ali Omar Chengo na Katibu wa tume hiyo ni Shaaban Ramadhan Abdalla. Uteuzi huo ulianza Julai 23, mwaka huu.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema tume hiyo imepewa muda gani wa kukamilisha uchunguzi huo.

WAZIRI MPYA ATEULIWA
Katika hatua nyingine, Rais Shein amemteua Rashid Seif Suleiman, kuwa Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasiliano kufuatia kujiuzulu aliyekuwa Waziri  wa Wizara hiyo, Hamadi Masoud, baada ya kuzama kwa boti hiyo.

Rashid ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la (Ziwani) alitarajia kuapishwa Ikulu Zanzibar jana Alasiri kushika wadhifa huo.

Wakati huo huo; Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi jana walimpokea kwa kishindo Rashid muda mfupi baada ya kuingia katika ukumbi kufutia kuteuliwa kwake.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir kificho, alilazimika kuachia kwa muda shangwe za makofi wakati wajumbe walipokuwa wakihoji taarifa ya serikali juu ya kuzama.

WAZIRI APONGEZWA KWA KUJIUZULU
Kujiuzulu kwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa ya Zanzibar, Hamad Masoud Hamad, kumepongezwa na makundi kadhaa ya jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema hatua hiyo ni nzuri kama waziri mwenye dhamana kwa kuwa inaonekana kuna tatizo la utawala kutokana na kujirudia kwa tatizo hilo la kuzama kwa vyombo vya usafiri na kwamba isingekuwa vyema kuendelea kubaki kwenye nafasi yake.

“Amechukua hatua nzuri kama waziri mwenye dhamana hasa ikizingatiwa ni muda mfupi tu umepita tangu kuzama kwa meli nyingine na kuua Watanzania wengi,” alisema.

Dk. Bisimba aliongeza kuwa waziri huyo anahitaji pongezi nyingi kwa hatua hiyo kwa kuwa ni viongozi wachache nchini wenye ujasiri wa kufanya maamuzi kama hayo.

Aliitaka serikali kufanya uchunguzi zaidi ili ijue chanzo na wahusika wa ajali hiyo ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya,  alisema hatua aliyochukuwa waziri huyo ni sahihi kwa nchi yoyote inayotaka kujenga utawala bora hasa kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia na kwamba serikali itumie hatua hiyo kama chachu ya kuwajibika zaidi.

“Kwa nchi yoyote inayotaka kujenga utawala bora, hii ni hatua sahihi, hatutarajii madudu kama haya yatokee tena zaidi ya mara moja halafu waziri mwenye dhamana aendelee kubaki kwenye nafasi yake, inaonekana kuna rushwa na uzembe ndani ya hii ajali,” alisema.

Naye Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Daar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema hatua ya kujiuzulu kwa waziri huyo ni nzuri na inayohitaji pongezi kwa kuwa amechukua maamuzi magumu ya uwajibikaji kwa vitendo kwa kubeba dhamana ya wizara yake.

“Huyu waziri anahitaji pongezi kwa sababu amechukua maamuzi magumu ya kuonesha uwajibikaji kwa vitendo kwa kukubali kubeba dhamana ya wizara yake hata kama hajahusika moja kwa moja kwenye ajali hiyo, ni viongozi wachache wenye ujasiri huo,” alisema Dk. Bana.

Alitoa wito kwa viongozi wengine katika wizara nyingine serikalini kuiga mfano huo wa uwajibikaji kwa vitendo, kwa kuwa tayari kuwajibika pale wizara zao zinapohusika na matukio yanayowagusa kwa namna moja au nyingine.

Dk. Azaveli Lwaitama, ambaye ni Mhadhiri mstaafu wa Filosofia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema: 

“Hatua hiyo imejenga sifa na hadhi nzuri kwa waziri huyo na hata kwa Rais wa Zanzibar kwa kukubali kujiuzulu kwake, ameonyesha mfano mzuri na anahitaji pongezi hata kama hajawajibika moja kwa moja kwenye suala hilo.”

Dk.  Lwaitama aliongeza kuwa kitendo cha waziri kujiuzulu haimaanishi kwamba amewajibika kwenye tukio hilo la ajali, lakini ni njia mojawapo ya kujijengea heshima na uaminifu kwa wananchi.


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, alisema hatua aliyochukua Waziri Hamad ni ya uwajibikaji kisiasa japokuwa hakuhusika yeye binafsi katika ajali hiyo na kwamba kujiuzulu kwake kumeonyesha kwamba CUF ni chama makini.



“Kujiuzulu kwake kunadhihirisha umakini wa chama cha CUF, Hamad alikuwa mmoja kati ya mawaziri wawajibikaji wazuri na nina uhakika Rais Shein atamkumbuka sanakwa hilo,” alisema Prof. Lipumba.

Waziri Hamad  alijiiuzulu wadhifa wake Julai 20, mwaka huu, kufuatia ajali ya Mv Skagit iliyozama na kupinduka katika kisiwa cha Chumbe Julai 18, mwaka huu.

MAITI 11 ZAOPOLEWA
Wakati huo huo, miili ya watu 11 wa ajali hiyo iliopolewa jana jioni na kuongeza idadi ya maiti zilizopatikana kufikia 92.

Hata hivyo, bado watu 52 waliokuwemo ndani ya boti hiyo hawajulikani waliko.


Habari na MWINYI SADALLAH
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa