na Mauwa Mohammed, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema sekta ya uvuvi inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo migogoro baina ya wavuvi, wakulima wa mwani na wawekezaji waliowekeza katika sekta ya utalii.
Hayo yalibainika jana wakati Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdillahi Jihadi Hassan, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Jihadi alisema migogoro mingine ni kuongezeka shinikizo la uvuvi katika maeneo ya hifadhi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wavuvi na kusababisha uharibifu wa matumbawe unaotokana na kukwamisha nyavu chini ya bahari.
“Hali hiyo huchangia uharibifu wa makazi ya samaki unaosababishwa na matumizi ya uvuvi haramu wa nyavu za macho madogo, nyavu za kukokota na mfumo mbaya wa mitego inayobuniwa na wavuvi ambayo inavua samaki wachanga,” alisema.
Aidha, alisema uwezo mdogo wa jamii wa kuwekeza katika ufugaji wa mazao ya baharini kutokana na gharama kubwa za uwekezaji na uhaba wa taaluma katika fani ya ufugaji wa mazao ya bahari.
Hata hivyo, alisema wizara ipo katika jitihada za kuongeza wataalamu wa fani ya ufugaji wa mazao ya baharini pamoja na kuhamasisha uvuvi wa kina kirefu cha maji na kufanya tafiti, ili kutambua maeneo mapya ya uvuvi.
Katika kutekeleza mipango iliyojiwekea wizara hiyo Waziri Jihadi alisema wizara yake imekamilisha utayarishaji wa sera ya mifugo na kuzifanyia mapitio sheria ndogo ndogo za mifugo na uvuvi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment