Sekta binafi visiwani Zanzibar imelalamikia ongezeko la gharama za umeme kwa zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na gharama za Tanzania Bara. Pamoja na hilo, nishati hiyo bado pia imekua sio ya uhakika kutokana na miundombinu yake ya usambazaji kuwa mibovu.
Katika mkutano uliofanyika baina ya sekta binafsi na sekta ya umma ulioongozwa na Shirika la Kitaifa la Zanzibar la Biashara, Viwanda na Kilimo (ZNCCIA), imebainika kuwa gharama kubwa za umeme na upatikanaji wake usiokuwa wa uhakika ni kikwazo kikubwa kinachozuia uboreshaji wa mazingira ya biashara visiwani humo.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa ZNCCIA, Bw. Ali Aboud na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Bi. Munira Hamoud, walisema, gharama kubwa za nishati ya umeme sio tu kuwa zinawaumiza watumiaji wa kawaida bali pia zinaweza kuzorotesha uzalishaji viwandani.
Viongozi hao pia walibainisha kuwa kuongezeka kwa gharama hizo za umeme kutasababisha mfumuko wa bei visiwani humo na hivyo kusababisha kuongezeka kwa gharama za kuendeshea biashara.
Dk. Mohammed Hafidh Khalfan, ni mwanauchumi maarufu, ambaye amepewa jukumu na ZNCCIA chini ya programu ya BEST-AC kuangalia masuala hayo alisema:
“Gharama za umeme ndio kikwazo kikubwa cha mendeleo ya biashara, uendeshaji na ukuaji wake visiwani Zanzibar. Bila kuwa na suluhisho la kudumu la kutatua kikwazo hiki, ndoto ya Zanzibar ya kuwa na uchumi wa tabaka la kati ifikapo mwaka 2020 haitafikiwa, badala yake hali itakuzidi kuwa mbaya. "
Dk. Khalfan ametoa maoni yake kuwa Zanzibar ina uwezo wa kuvutia uwekezaji mkubwa lakini gharama za uzalishaji zinazosababishwa na tatizo la umeme miongoni mwa matatizo mengine, limepoteza matumaini ya kuweza kuyafikia malengo yaliyobainishwa katika Sera ya Uwekezaji ya Zanzibar.
“Athari za gharama kubwa za umeme zinaweza kukisiwa na kupata picha halisi: gharama kubwa za umeme huchangia kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, na pia hupunguza uzalishaji na faida kwa mfanyabiashara," alisema
Gharama mpya za umeme
Shirika la Umeme visiwani Zanzibar (ZECO) kuanzia tarehe 1 Juni mwaka huu liliongeza bei za umeme kama ifuatavyo: gharama kwa watumiaji wa kawaida (ikiwa ni pamoja na watumiaji wa umeme majumbani) imekua sh. 161 / - kutoka sh. 120 / -, Viwanda vidogo (imekua sh. 172 / - kutoka sh. 140 / -), viwanda vikubwa (imekua sh. 169 / - kutoka sh. 142 / -), na taa za barabarani (imekua sh. 141 / - kutoka sh.105 / -). Gharama za huduma kwa wateja zimeongezeka kutoka sh. 1,500 - hadi sh. 2,000.
Athari za ongezeko la gharama za umeme
ZNCCIA inabainisha kuwa gharama za umeme zilizoongezeka hazina tija kwa wafanyabiashara na biashara zao.
-Nyongeza hiyo ya gharama za umeme inaweza kufukuza wawekezaji wenye kuleta tija visiwani humo.
-Ongezeko hilo pia litavuruga uwezo wa uzalishaji viwandani, utasababisha upotevu na kutotumika kwa rasilimali zilizopo.
- Ongezeko hilo pia litasababisha kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa toka nje na hivyo utaongeza uhitaji mkubwa wa fedha za kigeni
- Ongezeko hilo pia litaua viwanda vilivyobakia visiwani humo taratibu ambavyo bado vingali vichanga
Changamoto
Kisiwa cha Unguja mjini Zanzibar kiliunganishwa na gridi ya taifa mnamo mwaka 1980 kwa msongo wa 132kV 45MW ambao umepitishwa chini ya bahari na bado unatumika licha ya muda wake wakufanya kazi kumalizika.
-Ni mwezi Mei tu mwaka 2010, kisiwa cha Pemba kiliunganishwa na gridi ya taifa kutoka Tanga kupitia chini ya bahari, lakini gharama za umeme na upatikanaji wake bado ni changamoto kubwa.
Kwa siku zijazo, ZNCCIA inazitaka sekta binafsi ziwe zinashirikishwa kikamilifu kutoa ushauri kama mteja mkubwa wa umeme kabla ya kupanga na kuanzisha gharama mpya.
ZECO ni shirika la umma linalojitegemea, na linapata nishati yake ya umeme kutoka TANESCO. Shirika hili limekuwa likipata hasara kwa miaka kadhaa sasa, na limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi kutokana na miundombinu yake ya usambazaji umeme kuwa mibovu, malimbikizo makubwa ya bili za umeme kwa baadhi ya taasisi zilizosababisha hasara na wizi wa umeme.
Nafasi ya ZNCCIA katika suala hili ni kwamba, serikali inashughulikia matatizo hayo kwa kuiboresha ZECO na kuanza kufanya kazi katika mipango yake ya muda mrefu kwa ajili ya kuweza kujitegemea na kuzalisha umeme kwa gharama nafuu ili kupunguza utegemezi kutoka shirika la umeme, TANESCO.
Kuhusu ZNCCIA
Shirika la Taifa la Zanzibar la Biashara, Viwanda na Kilimo (ZNCCIA) ni sekta binafsi mwanachama iliyosajiliwa visiwani Zanzibar.
ZNCCIA inakusudia kuchochea ukuaji wa biashara visiwani Zanzibar kwa kutoa mapendekezo mazuri yaliyotengenezwa ili kuondoa vikwazo vinavyoikabili jamii hususani katika masuala ya biashara, viwanda na kilimo; kukuza umoja wa wadau katika sekta binafsi, kuwezesha makampuni ya biashara ya Zanzibar kupata ujuzi, soko, ushirikiano, fursa za uwekezaji na rasilimali fedha. ZNCCIA pia inajitahidi kushirikiana na serikali ili kuifanya Zanzibar ivutie zaidi wawekezaji.
----------------------------------------------
Kwa swali lolote au maoni, tafadhali wasiliana na:
Shirika la Taifa la Zanzibar la Biashara, Viwanda na Kilimo (ZNCCIA)
Mtu wa kuwasiliana nae: Mkurugenzi Mtendaji, ZNCCIA
Simu: 025 24 223 4713
Nukushi (Fax): 025 24 223 1710
Barua pepe (email): info@znccia.org
Tarehe: Agosti 7, 2012
0 comments:
Post a Comment